Jumia bado inaendelea na wingu lake la kusitisha baadhi ya biashara zake barani Afrika, baada ya kusitisha huduma zake nchini Cameroon na Tanzania takribani wiki mbili zilizopita, hapo jana kampuni hiyo imetangaza kusitisha huduma zake nchini Rwanda.
Kwa mujibu wa tovuti ya New Times Rwanda, Kampuni ya Jumia imatangaza kusitisha biashara yake ya usambazaji wa chakula ambayo ilikuwa ikifanyakazi kwenye nchi ya Rwanda kwa takribani miaka 6 hadi sasa. “Tuna sikitika kukujulisha kuwa Jumia itasimamisha shughuli zetu za utoaji wa mahitaji nchini Rwanda mnamo Januari 9, 2020,” ilisema sehemu ya taarifa kwa watumiaji wa huduma hiyo nchini Rwanda.
Pia kwenye taarifa hiyo, Jumia iliainisha kuwa hakuna oda yoyote itakayo shughulikiwa baada ya tarehe 9 Januari 2020, wakati ambao akaunti zote za wateja zitafungwa. Pia watoa huduma wakuu wa Jumia nchini humo watawasiliana na kampuni kuhusu malipo yao.
Vilevile kuanzia jana tarehe 9 desemba 2019, Jumia Rwanda ilitangaza kuwa haitopokea oda za malipo baada ya kufikisha (cash on delivery) na badala yake itakuwa inafanyia kazi oda ambazo zitakuwa zimelipiwa kabla (pre-paid orders).
Albert Munyabugingo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jumia kwa shughuli za Rwanda, aliliambia gazeti la The New Times kwamba Jumia Rwanda imekuwa “ikipata shinda kupata faida” katika masoko tofauti, ambayo ilisababisha kwa uamuzi wa kusimamisha shughuli kadhaa.
Kufungwa kwa Jumia Travel
Mbali na hayo, kwa mujibu wa tovuti ya TechCabal, Jumia imetangaza pia kusitisha huduma zake za Jumia Travel nchini Nigeria na badala yake huduma hizo zitachukuliwa na kampuni ya Travelstart.
“Tumeamua kuleta ushirikiano na mwenzi wetu, Travelstart. Wakati tukiendelea kukuza jamii ya Usafiri, kampuni ya Travelstart itawajibika kwa upande wa uendeshaji wa biashara, ” ilisema taarifa kutoka Jumia kwenda tovuti ya TechCabal.
Tovuti ya Jumia Travel itaelekeza wageni kwenye tovuti ya Travelstart kuanzia Jumatatu. Hata hivyo Haijulikani ikiwa “ushirikiano” unahusu biashara nzima ya Jumia Travel nchini humo kwani inasemekana karibu kila nyanja ya uendeshaji wa biashara hiyo itakuwa nje ya usimamizi wa Jumia. Inasemekana Apps pamoja na website zote za Jumia Travel zitasitishwa na hazitokwepo kabisa nchini humo.
Kwa upande wa Tanzania inaonekana pia Jumia Travel imefungwa, kutokana na Sehemu ya matangazo ya biashara kwenye tovuti ya Google kuonyesha biashara hiyo imefungwa rasmi.
Hata hivyo bado tovuti ya Jumia Travel inaweza kuonekana moja kwa moja bila kuonyesha ishara ya kuwa imefungwa. Tutafutatilia ili kupata uhakika wa hili na tutakupa taarifa zaidi kama Jumia Travel imesitishwa kwa Tanzania pia. Kwa habari zaidi hakikisha unaendelea kutembelea Tanzania Tech kila siku.