Wakati mtandao wa TikTok ukiendelea kuwekewa vikwazwo kwenye nchi kama India, YouTube imeona nafasi kwa kuzindua huduma yake mpya ya video fupi inayoitwa Shorts. Sehemu hii ni sehemu kama ilivyo TikTok lakini kwaajili ya mtandao wa YouTube.
Huduma hiyo mpya ambayo kwa sasa ipo kwenye hatua za majaribio huko nchini India, inawawezesha waundaji kuchukua video tofauti na kuziunganisha pamoja kwa kutumia seti ya zana za kuhariri zilizojengwa ndani ya sehemu hiyo mpya.
Mbali na hayo, waundaji wanaweza pia kuhariri video kwa kuongeza kasi ya video ikiwa pamoja na kuongeza muziki kwenye video zao kwa kutumia maktaba ya nyimbo kupitia mtandao wa YouTube.
Kama ilivyo TikTok, pia sehemu hiyo mpya ya Shorts itaruhusu watumiaji kuweza kuweka video fupi kuanzia sekunde 15, mbali na hayo Shorts pia inakupa uwezo wa kugundua video nyingine kwa kusegea kwa mtindo wa wima kama ilivyo kwenye mtandao wa TikTok.
Kwa mujibu wa YouTube, sehemu hiyo mpya ya Shorts itakuwa inapatikana ndani ya App ya mtandao wa YouTube lakini pia itapatikana kwenye mfumo wa iOS hivi karibuni. Kujua zaidi kuhusu sehemu hii hakikisha unaendelea kutembelea Tanzania Tech kila siku.