Kampuni ya Facebook kupitia programu yake ya WhatsApp, hivi karibuni imewataka watumiaji wake kuchukua hatua za haraka kusasisha (update) toleo jipya la programu hiyo kutokana na kugundulika kuwa matoleo yaliyopita ya programu hiyo kuwa na uwezo wa kudukuliwa (Hacked).
Kwa mujibu wa tovuti ya The Guardian, WhatsApp imegundua aina hiyo mpya ya udukuaji ambapo serikali inaweza kutumia programu zake za kiusalama kuweza kusoma meseji zote za WhatsApp pamoja na kuchukua data mbalimbali za utumiaji wa programu hiyo.
Hata hivyo ugunduzi huo unakuja baada ya WhatsApp kuweza kugundua programu ya uchunguzi (spyware) ambayo inasemekana imetengenezwa na Israeli Cyber Intelligence Company NSO Group, ambapo spyware hiyo inaweza kudukua programu hiyo ya WhatsApp pale mtumiaji anapo pokea voice call kupitia WhatsApp bila kujali kama mtumiaji amepokea simu au hajapokea.
WhatsApp inadai kuwa imegundua aina hiyo mpya ya udukuzi mwezi huu wa tano, na iliweza kufanya marekebisho kwenye miundombinu yake yote ya programu hiyo ndani ya kampuni ya WhatsApp. Vilevile whatsapp ilituma sasisho au update za programu hiyo siku ya jumatatu ya wiki iliyopita huku ikiwataka watumiaji ku-update programu hiyo haraka.
Kwa mujibu wa The Guardian, inasemekana udukuzi huo ulikuwa ukitaka kutumika dhidi ya simu ya wakili mmoja wa nchini uingereza siku ya May 12. Hata hivyo inasemekana kuwa wakili huyo alikuwa akihusika kwenye kesi inayo husisha kampuni hiyo ya Israeli ya NSO Group.
NSO Group ni kampuni ya israel ambayo inajiusisha na ulinzi wa kimtandao, kampuni hiyo iligunduliwa mwaka 2010 na inasemekana kuwa na wafanyakazi zaidi ya 500 huku ikiwa na mapato ya zaidi ya dollar za marekani milioni $150 ambayo ni sawa na takribani zaidi ya shilingi za Tanzania bilioni 344.
Kwa sasa WhatsApp inawataka watumiaji wote wa programu hiyo kuweza ku-update programu hiyo sasa ili kuweza kujikinga na udukuzi kama huu ambao umegundulika siku za karibuni. Kwa habari zaidi kuhusu hili endelea kutembelea Tanzania Tech tutakujuza zaidi pale tutakapo pata taarifa zaidi.