Najua utakuwa umeshtuka kidogo baada ya kuona kichwa cha habari lakini ni kweli, Inasemekana Facebook imepanga kufanya mabadiliko kidogo ya mitandao yake ya WhatsApp na Instagram ili kufanya watu wajue zaidi kama mitandao hiyo inamilikiwa na kampuni ya Facebook.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka tovuti ya engadget, hivi karibuni Facebook inategemea kubadilisha majina ya app hizo na kuweka jina la Facebook kwenye kila jina la application. Kwa mujibu wa ripoti hizo, inadaiwa kuwa WhatsApp itakuwa inaitwa “WhatsApp From Facebook” na Instagram itakuwa inaitwa “Instagram From Facebook”.
Inasemekana kuwa tayari Facebook imeshatoa maagizo kwa wafanyakazi wa kampuni zake hizo kuwataka kujua itaongeza jina lake kwenye App hizo. Hata hivyo inasemekana kuwa mmoja wa wasemaji wa kampuni ya Facebook ambaye akutajwa jina alisibitisha mabadiliko hayo kwa kusikika akisema kuwa, “Tunataka kuwa wazi juu ya bidhaa na huduma ambazo ni sehemu ya Facebook.”
Ni wazi hadi sasa watu wengi hawajui kama programu za WhatsApp na Instagram zinamilikiwa na Facebook, hivyo kama lengo la Facebook ni kutaka hilo kujulikana basi ni wazi hatua hii itafanya watumiaji wa Instagram na WhatsApp kote duniani kujua kwamba programu hizi zinamilikiwa na Facebook.
Kwa sasa bado hakuna taarifa kamili za uhakika kuhusu mabadiliko hayo ya majina yatafanyika sehemu gani hasa, lakini huwenda mabadiliko hayo yakafanyika zaidi kwenye masoko ya Play Store na App Store na sio kwenye App zenyewe. Inasemekana mara baada ya Facebook kuachana na waanzilishi wa programu hizo za Instagram na WhatsApp sasa inataka kuweka wazi kuwa inamiliki App hizo kwa asilimia 100.
Bado haijajulikana mabadiliko hayo yatafanyika lini lakini tegemea kuona mabadiliko hayo siku za karibuni. Kujua zaidi kuhusu hili hakikisha unaendelea kutembelea tovuti ya Tanzania Tech tutakujuza yote yatakayo endelea.