Mwaka jana 2018, tulitengeneza makala inayohusu jinsi ya kuuza bidhaa kupitia WhatsApp. Pengine tuliwaza kabla ya Facebook lakini kwa vyovyote sasa nadhani makala hiyo itakuwa imepitwa na wakati kidogo. Hii ni kwa sababu sasa utaweza kuuza au kuonyesha bidhaa zako kupitia WhatsApp ya biashara bila kuhitaji app nyingine ya ziada.
Kama ulifanikiwa kusoma makala hiyo, ili kuweza kuuza bidhaa kupitia WhatsApp ilikuwa ni lazima kuinstall app nyingine ya ziada lakini kwa sasa hiyo sio lazima.
Kupitia sehemu mpya ya Catalog ndani ya WhatsApp ya biashara, utaweza kuonyesha bidhaa zako moja kwa moja kupitia app ya WhatsApp Business na wateja wataweza kuona bei ya bidhaa zako, maelezo mafupi kuhusu bidhaa, pamoja na link ya kununua bidhaa kama utakuwa unauza kupitia mtandao pamoja na maelezo mengine.
Kwa mujibu wa blog ya WhatsApp, sehemu hii imewekwa ili kusaidia wafanya biashara wadogo kuweza kufikia wateja wao kwa urahisi na haraka bila kupata usumbufu wa kuchat na kutumia picha kwa muda mrefu kabla ya mteja kuweza kununua bidhaa. Pia kupitia Catalog utaweza kutuma bidhaa kwa mteja kwa haraka na urahisi zaidi.
Ili kuonyesha bidhaa zako kupitia WhatsApp ya Biashara unaweza kufuata hatua hizi fupi. Ingia kwenye App yako ya WhatsApp ya Biashara, kisha bofya sehemu ya Settings > Business settings > kisha bofya Catalog. Baada ya hapo bofya sehemu ya Add Product or Service baada ya hapo utaletewa ukurasa utakao kusaidia kuweka bidhaa, chagua picha, weka maelezo ya bidhaa, link pamoja na bei kisha ukimaliza bofya Save.
Kwa sasa sehemu hii inapatikana kwenye programu ya WhatsApp business na unaweza kuanza kutumia sehemu hiyo sasa. Kama kwa namna yoyote utakuwa hujaona sehemu ya Catalog kwenye WhatsApp Business hakikisha una sasaisha toleo jipya la kupitia soko la Play Store au App Store. Kama bado huna app ya WhatsApp ya biashara unaweza kupakua app hiyo kupiti link hapo chini.
Kwa habari zaidi za teknolojia hakikisha unaendelea kutembelea Tanzania Tech kila siku, kama unataka kupata habari wa kwanza hakikisha unapakua app Tanzania Tech kupitia soko la Play Store..