Ni wazi kuwa kunalo ongezeko kubwa sana la watalaam mbalimbali hivyo, kwa mujibu wa gazeti la Habari leo limeandika kuwa, Kutokana na ongezeko la matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema kuna umuhimu wa kuanzisha bodi itakayo watambua wataalam wa sekta hiyo.
Mhandisi Nditiye amesema hayo bungeni, Dodoma leo asubuhi wakati akijibu swali la mbunge wa Busekelo, Atupele Mwakibete ambaye, pamoja na mambo mengine, alitaka kujua iwapo kuna mpango wa kuundwa kwa bodi ya wataaluma waliosomea TEHAMA hata kuwa na bodi yao.
Naibu Waziri amesema Sera ya Taifa ya TEHAMA ya Mwaka 2016 inatamka umuhimu wa “kuwepo kwa mfumo wa kuwatambua na kuwaendeleza wataalam wa TEHAMA ili kuwa na rasilimali watu ya kutosha nchini ambayo inazingatia maadili yenye uwezo wa kufanikisha jitihada za sekta hiyo katika kujenga jamii maarifa.”
Amesema kuwa tamko la Rais la Novemba, 2016, limeanzisha Tume ya TEHAMA (ICT Commission) ikiwa na lengo kuu la kuikuza sekta hiyo ambayo moja ya majukumu yake ni kusajili, kusimamia na kuendeleza wataalam. Ameongeza kuwa kupitia tume hiyo, serikali inaangalia uwezekano wa kuunda bodi itakayo watambua wataalam wote wa TEHAMA kwa elimu zao na hata kufanya mitihani kama zilivyo taaluma kama uhasibu na nyingine.