Mitandao ya kijamii kwa sasa imekuwa ni sehemu kubwa ya utambulisho binafsi wa mtu, ndio maana kwa mujibu wa tovuti ya VOA, Takriban kila mtu atakaye omba visa ya kuingia Marekani atatakiwa kutoa akaunti zake za mitandao ya kijamii pamoja na taarifa zingine binafsi kama sehemu ya utaratibu mpya wa Marekani wa kuhakiki wahamiaji na wageni wote.
Kwa mujibu wa tovuti hiyo, Wizara ya mambo ya nje ya Marekani inaeleza kwamba imefanya mabadiliko kwenye fomu za kuomba visa kwa wahamiaji na wasio wahamiaji zikimtaka muombaji kutoa taarifa za miaka mitano iliyopita za shughuli zao kwenye mitandao ya kijamii, nambari ya simu, barua pepe, safari za kimataifa na ikiwa kama amewahi kufukuzwa kutoka nchi hiyo. Pia wataulizwa iwapo mwanafamilia yeyote amehusika katika kazi za ugaidi.
Kwa mujibu wa TechCrunch, Utaratibu huu mpya ulipendekezwa kwanza mwaka 2018 na unatarajiwa kuathiri takribani zaidi ya watu milioni 15, ikiwemo watu wanao omba kuingia Marekani pamoja na wale wenye matumaini ya kusoma, kufanya biashara, kazi au kuingia nchini humo kwa ajili ya kutembea.
Hata hivyo inasemekana kuwa, waombaji wa Visa za kidiplomasia na visa rasmi pekee ndio ambao hawatahusishwa na utaratibu huo mpya. Kama wewe unayo akaunti yoyote ya mtandao wa kijamii sasa kuna haja ya kuwa makini na vitu unavyoweka kwenye akaunti zako za mitandao ya kijamii kwani kwa sasa inaonekana kama ni sehemu muhimu sana ya kuweza kujua tabia ya mtu.