Mlipuko wa virusi vya corona au coronavirus bado unaendelea kuwa tishio kwa dunia na wakati virusi hivyo vikiendelea kusambaa duniani, kampuni ya Apple imetengaza kufunga ofisi zake pamoja na maduka yake yote 42 nchini China kutokana na mlipuko wa virusi hivyo.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa wiki iliyopita, Apple imetengaza kufunga maduka yake hayo pamoja na ofisi hadi tarehe 9 ya mwezi huu ikiwa ni siku tatu tu zimebaki hadi kufikia kikomo hicho. Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali mtandaoni, inasemekana kuwa Apple haitoweza kufungua maduka yake na ofisi nchini humo kutokana na kuendelea kusambaa kwa mlipuko wa virusi hivyo vya coronavirus.
Mbali na ofisi pamoja na maduka, pia moja ya kiwanda kikubwa cha uzalishaji wa simu za Apple nchini China Foxconn, nao pia wametangaza kusitisha kazi zake hadi tarehe 10 mwezi huu ikiwa pia ni hatua ya kulinda wafanyakazi wake kutokana na virusi hivyo hatari vya corona.
Hata hivyo kampuni ya Apple inasemekana tayari inategemea kupata hasara kutokana na kile kinachotabiriwa kuwa ni kushuka kwa uzalishaji hadi asilimia 10 kutokana na kuwa Foxconn ndio wazalishaji wakubwa wa simu za iPhone.
Mbali na kampuni ya Apple, kampuni nyingine kama ZTE na LG hivi leo zimetangaza kujitoa kwenye mkutano wa MWC 2020 ambao unategemea kuanza tarehe 24 mwezi huu huko nchini Barcelona, huku sababu kubwa ya kujitoa huko ikiwa ni kusambaa kwa virusi hivyo vya corona.
Kampuni ya LG imetangaza kuwa, inategemea kuwa na mkutano wake baadae mwaka huu kwa ajili ya kutangaza bidhaa zake mpya kama ilivyo tarajiwa kwenye mkutano wa MWC ambao hufanyika kila mwaka. Kwa sasa GSMA ambao ndio waandaji wa mkutano huo wametangaza kuwa mkutano huo utaendelea kama kawaida huko nchini Barcelona kuanzia Jumatatu, Feb 24, 2020 hadi Alhamisi, Feb 27, 2020.