Viongozi wakubwa wa nchini marekani ambao ni viongozi wa FBI, CIA, pamoja na NSA wameonya juu ya utumiaji wa simu za Huawei na ZTE nchini marekani.
Ripoti kutoka tovuti ya CNBC, zinasema kuwa viongozi hao wamesema hayo kupitia mkutano wa Senate Intelligence Committee hearing ambao ulifanyika siku ya Jumanne na waliongoza mkutano huo walikuwa viongozi wa FBI, CIA, NSA pamoja na mkurugenzi wa usalama wa taifa wa marekani (director of national intelligence).
Wakati wa ushuhuda wake, Mkurugenzi wa FBI Chris Wray alisema ”serikali ina mashaka sana juu ya hatari za kuruhusu kampuni yoyote au taasisi za serikali za kigeni zisizo ruhusu serikali ya marekani kupata nafasi ya kujua data za mitandao ya mawasiliano ya watumiaji wake na hii itatoa nafasi kwa kampuni hizo kuiba taarifa za siri za watumiaji wake bila serikali ya marekani kujua au kuweza kuzuia.
Hata hivyo hatua hii inakuja baada ya kampuni ya Huawei kutangaza kupanua soko la simu zake huku ikitaja kuanza kuwafikia rasmi wateja wake wa nchini marekani hivi karibuni.
Huawei kupitia msemaji wake ilitoa maoni yake na kusema kuwa inajua lengo la viongozi hao kutaka kuzuia biashara ya Huawei katika soko la Marekani huku ikiwataka wateja wake kutokuwa na wasiwasi kwani Huawei ina aminika na wateja kwenye nchi 170 ulimwenguni kote na huko simu hizo hazina hatari yoyote ya usalama.