Habari kutoka tovuti ya gazeti la kila siku la Mwananchi zinasema kuwa, Mabasi 29 ya mradi wa mabasi yaendayo haraka (Udart) yameharibika kutokana na eneo lake la maegesho kujaa maji yanayotokana na mvua zinazoendelea kunyesha hapa jijini Dar es salaam.
Maegesho ya mabasi hayo yaliyopo eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam hujaa maji kila inaponyesha mvua kubwa. Mbali ya mabasi, pia baadhi ya wafanyakazi wamepewa likizo mpaka maegesho mengine ya mabasi hayo yatakapopatikana.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 7, 2018 Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano wa Udart, Deus Bugaywa amesema kujaa kwa maji eneo hilo kumesababisha shughuli mbalimbali kusimama jambo lililowafanya waanze kutafuta eneo lingine la kufanyia kazi.
Amesema moja ya sababu iliyochangia hali hiyo ni sehemu ya ukuta ya eneo hilo kudondoka na hivyo maji ya Mto Msimbazi kuingia ndani kwa wingi. Amesema matengenezo ya mabasi hayo yanafanyika eneo la maegesho ya muda katika vituo vyao vya Gerezani, Kivukoni na Kimara wakati wakiendelea kutafuta sehemu nyingine.
Siku za karibuni ilisemekana kuwa, Serikali imempata mwendeshaji wa pili wa mradi wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam (DART), baada ya mwendeshaji wa kwanza wa mradi huo kuonekana kusuasua, hivyo labda tutegemee kuona mabadiliko ya sehemu mpya itakayo tumika kuegesha magari hayo pamoja na ufanisi zaidi wa mabasi hayo pamoja na Kampuni ya (Uda-RT) kwa ujumla.
Imenakiliwa Kutoka Tovuti ya Mwananchi na Kuhaririwa na Tanzania Tech
Nice