Baada ya miaka mitatu Twitter kutangaza kusitisha hatua za kuthibitisha akaunti mbalimbali, hivi karibuni kampuni hiyo imetangaza kuanza tena kuthibitisha akaunti kuanzia mapema mwaka 2021.
Mbali na kuthibitisha akaunti, Twitter pia imesema kuwa inategemea kuleta aina mpya za akaunti, ikiwa pamoja na label au vitambulishi vipya vya akaunti kupitia mtandao huo.
Kulingana na sera iliyopendekezwa ya uthibitishaji, Twitter itafungua maombi ya uthibitishaji kwa aina zifuatazo za akaunti: akaunti za serikali, akaunti za kampuni, chapa na mashirika yasiyo ya faida, habari, burudani, michezo, wanaharakati, waandaaji, na watu wengine wenye ushawishi.
Mbali na hayo, Twitter imeelezea mahitaji maalum ya kuhakikiwa katika sera yake ya rasimu. Kwa mfano, kampuni inatakiwa kuwa na tovuti iliyo na kitambulisho kilichothibitishwa, kampuni hiyo pia iwe inatambulika na iwe imeshawahi kutangazwa kwenye media yoyote inayotambulika ndani ya miezi sita iliyopita na mambo mengine mengi. Unaweza kusoma sera hio na mahitaji hayo hapa.
Twitter pia imeandika kwenye blog yake kuwa, zipo akaunti nyingi ambazo kwa sasa zimethibitshwa lakini hazisitahili kuwa na uthibitisho huo, hivyo ili kuhakikisha hatua hii haitokei tena kampuni hiyo inatarajia kuanza kuondoa alama ya uthibitisho (Verified Badge) kwenye akaunti ambazo zinakiuka masharti ya mtandao huo, ikiwa pamoja na akaunti ambazo hazitumiki kwa muda mrefu.
Kwa sasa Twitter inafanya utafiti maalum kuhusu sheria na vigezo vya uthibitishaji huo kabla ya kutangaza rasmi sheria na vigezo vitakavyo kuwa vinatumika kuthibitisha akaunti mbalimbali. Unaweza kushiriki kwenye utafiti huo kupitia hapa kabla ya tarehe 8 disemba, ambapo sheria hizo zinatarajiwa kutangazwa rasmi tarehe 17 disemba mwaka huu 2020.