Habari mpya hivi leo zinasema kuwa, mtandao wa Twitter umedukuliwa na akaunti za kampuni kubwa na watu maarufu kutumika kufanya utapeli.
Kwa mujibu wa mtandao huo, akaunti za kampuni hizo na watu maarufu ni pamoja na Raisi mstaafu wa marekani Barack Obama, Joe Biden, Elon Musk, Bill Gates, Kanye West, Michael Bloomberg, pamoja na akaunti ya kampuni ya Apple.
Twitter imethibitisha kuwa ilichukua hatua kali ya kuzuia tweets mpya kutoka kwa kila mtumiaji aliyethibitishwa (Verified), ikiwa pamoja na kufunga akaunti zote zilizozudukuliwa.
Hata hivyo, Twitter ilitangaza kuwa haito rudisha akaunti hizo kwa watumiaji wake mpaka pale itakapo hakikisha kuwa akaunti hizo ziko salama kwa asilimia 100.
Hata hivyo inasemekana kuwa baadhi ya miundo mbinu ya ndani ya kampuni ya Twitter ilitumika kutekeleza udukuaji huo, ndio maana inasemekana kuwa akaunti za watu maarufu ambazo pia zilikuwa na ulinzi wa ziada (two-factor authentication) nazo pia ziliweza kudukuliwa.
Kwa sasa inasemekana baadhi ya akaunti tayari zimeanza kuruhusiwa kutweet, huku Twitter ikiendelea kufuatilia na kuongeza ulinzi wa akaunti hizo.
Inasemekana Akaunti ya kwanza kudukuliwa ilikuwa ni akaunti ya CEO wa kampuni ya Tesla, ambapo wadukuaji walikua wakifanya utapeli kwa kutumia mtandao wa Bitcoin, huku wakiwataka wafuasi wa akaunti hiyo kutuma pesa kupitia Bitcoin na baadae warudishiwe mara mbili ya pesa walizotuma kupitia Bitcoin. Unaweza kuona baadhi ya Tweets hizo kupitia hapo chini.
Kwa sasa bado Twitter inaendelea na uchunguzi ili kujua udukuzi huu umefanyika na nani au kikundi gani cha watu. Kwa taarifa zaidi endelea kutembelea Tanzania Tech.