Japokuwa ilianza kama kiwanda cha karatasi, kampuni ya Nokia imejizolea umaarufu mkubwa kwa utengenezaji wa simu ikiwa pamoja na smartphone, mbali na hayo kampuni hiyo imekuwa ikifanya biashara mbalimbali ikiwa pamoja na kuuza vifaa vya mawasiliano, lakini kama haitoshi hivi karibuni kampuni ya Nokia inategemea kuingia kwenye biashara nyingine mpya TV.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, Nokia inategemea kuingiza sokoni TV yake ya kwanza ambayo inasemekana kuwa Smart TV ambayo inategemewa kuzinduliwa rasmi siku ya Alhamisi ya wiki hii tarehe 5 mwezi wa 12 mwaka 2019 huko nchini India.
Kwa mujibu wa Techradar, Nokia inashirikiana na kampuni za Flipkart ya nchini India, pamoja na kampuni ya marekani ya JBL ambayo ni maarufu kwa utengenezaji wa vifaa vya sauti ikiwa pamoja na spika za sauti kubwa (Loudspeaker) pamoja na spika za kichwani maarufu kama headphone.
Kwa mujibu wa tovuti hiyo, inasemekana TV hiyo ya Nokia itazinduliwa kwanza nchini India na baadae kusambaa dunia nzima. Hata hivyo inasemekana kuwa TV hizo zitakuwa zinatengenezwa nchini India na kampuni ya Skyworth India Electronics pamoja na Skyquad zote za nchini humo.
Hata hivyo ripoti zinasema kuwa, Nokia inategemea kuzindua TV hiyo kwa toleo moja la inch-55 ambapo pia TV hiyo inasemekana kuwa na resolution ya hadi 4K. Kwa upande wa bei inasemekana TV hiyo ambayo ni Smart TV inategemea kuuzwa kwa Rupee ya India Rs. 40,000 ambayo ni sawa na takribani shilingi za Tanzania TZS 1,282,000 bila kodi.
Kwa sasa bado hakuna taarifa zaidi kuhusu TV hiyo, lakini kwa upande mwingine inasemekana pia Nokia inategemea kuzindua simu mpya ya bei nafuu ambayo itazinduliwa sambamba na TV hiyo. Kwa habari zaidi kuhusu hili hakikisha unaendelea kutembelea Tanzania Tech tutakupa habari yote yatakayojiri kwenye uzinduzi huo.
Nawatakia kila utekelezaji mwema katika utengenezaji wa tv bora na imara