Wakati kampuni ya Samsung ikijiandaa na ujio wa simu mpya ya Galaxy M40, tayari tetesi zimeanza kusambaa mtandaoni kuhusu simu mpya ya Galaxy Note 10 ambayo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi kati ya mwezi wa nane au wa tisa mwaka huu 2019.
Kwa mujibu wa tetesi mpya kutoka tovuti ya gsmarena, inasemekana kuwa simu hiyo mpya itakuwa na kamera moja kwa mbele, tofauti na simu za Galaxy S10 ambazo zenyewe zinakuja na kamera zaidi ya moja kwa mbele.
Mbali na hayo, Galaxy Note 10 inategemea kutoka kwa matoleo mawili tofauti ya Galaxy Note 10 na Galaxy Note 10 Pro huku simu zote zikisemekana kuwa na uwezo wa mtandao wa 5G. Kwa nyuma simu hizo zinasemekana kuja na kamera tatu pamoja na flash LED.
Kama unavyoweza kuona picha hapo juu, Galaxy Note 10 inakuja na muundo ambao unafanana kwa mbali na Galaxy S10. Hata hivyo kitu kingine ambacho ni tofauti kwenye simu hiyo ni kamera ya mbele ambayo sasa inasemekana kuwa katikati na sio pembeni kama simu za awali za Galaxy Note, pia kamera za nyuma zipo kwa mtindo wa kusimama tofauti na kwenye simu za awali ambapo zipo kwa mtindo wa mlalo.
Kwa sasa hayo ndio machache kuhusu Galaxy Note 10, kama unataka kujua zaidi kuhusu simu hii hakikisha unaendelea kutembelea tovuti ya Tanzania Tech kila siku na pia usisahau ku-subscrine kwenye channel yetu ili kujifunza maujanja mbalimbali kwa vitendo.