Kampuni ya Samsung ni moja kati ya kampuni ambazo zimekua na ubunifu wa kipekee wa kuja na simu zenye teknolojia za kisasa. Mara baada ya kuzindua simu mpya za Galaxy S10 zenye kamera za kisasa zilizopo juu ya kioo, kwa sasa ni wakati wa simu mpya za Galaxy Note 10.
Kwa mujibu wa tovuti ya nchini korea ya ETNews, Galaxy Note 10 inatarajia kuja na ubunifu mwingine wa kisasa ambapo sasa simu hizo zitakuja bila kitufe chochote cha kubonyeza na badala yake inasemekana kuwa Samsung inatarajia kutumia aina mpya ya teknolojia kama ile inayopatikana kwenye simu za HTC U12+.
Inawezekana kuwa simu hiyo itakuwa na teknolojia hiyo ya kugusa kwa pembeni kama mtu unataka kuongeza sauti au kupunguza, na pia kama unataka kuwasha simu hiyo. Kwa sasa bado hakuna taarifa zaidi kuhusu sehemu hiyo, ila inasekana bado kampuni ya Samsung inatafuta kampuni bora itakayoweza kutengeneza Sensor bora kwa ajili ya kufanya sehemu hiyo kufanya kazi vizuri zaidi.
Kwa habari zaidi kuhusu simu hii mpya ya Galaxy Note 10, pamoja na kujua lini simu hii itatoka hakikisha unaendelea kutembelea Tanzania Tech kila siku.