Programu ya Telegram ni moja ya programu maarufu ya kuwasiliana, mbali na kuwasiliana programu hii ni maarufu hasa upande wa channels au magroup mbalimbali.
Habari mpya hivi karibuni zinasema, kampuni ya Telegram imetangaza sehemu mpya kwa watumiaji wake ambayo itasaidia watumiaji wake kutengeneza pesa moja kwa moja kupitia kwenye app ya Telegram.
Kwa mujibu wa ripoti kupitia blog ya Telegram, watumiaji wa mtandao huo sasa wataweza kutengeneza pesa kwa kuwahitaji watumiaji wa channel mbalimbali kulipia kiwango kidogo kabla ya kuweza kuunganishwa na channel.
Kwa mujibu wa Telegram, watumiaji wataweza kulipia kujiunga na channel kwa kupitia fedha za kidigital za telegram maarufu kama “Stars”. Wamiliki wa channel wanaweza kutengeneza link maalum na kuweka kiwango cha Star wanachotaka ili mtumiaji aweze kulipia.
Ili kupata pesa, mmiliki wa channel unaweza kubadilisha kiwango cha “Stars” kuwa Toncoin cryptocurrency rewards au unaweza kutumia pesa hizo kwenye matangazo. Telegram huchukua kamisheni kutoka kwenye miamala hiyo ya “Stars”, ingawa bado kampuni hiyo haijataja ni kiasi gani.
Mbali na hayo kampuni hiyo pia imekuja sehemu mpya ya “Star Reactions”, sehemu ambayo inafanana na sehemu ya “Super Thanks” kupitia YouTube ambapo mtumiaji anaweza kutoa shukrani kwa kutuza fedha moja kwa moja kwa anae andaa maudhui au mmiliki wa channel.
Tangazo la leo linakuja wakati Telegram ilifikia watumiaji hai milioni 950 mwezi uliopita, na inalenga kuvuka watumiaji zaidi ya bilioni 1 mwaka huu.