Kampuni ya Tecno hivi karibuni imezindua simu mpya za Tecno Spark 3 na Spark 3 Pro huko nchini Nigeria. Lakini kama hiyo haitoshi kampuni hiyo inajiandaa na ujio wa simu nyingine ya Tecno Camon ambayo inakuja na kamera tatu kwa nyuma.
Kwa mujibu wa tovuti ya 91mobile, kwa sasa simu hiyo imesha zinduliwa rasmi huko nchini India kwa jina la tofauti la Tecno Camon i4. Kama ilivyo zoeleka kampuni ya Tecno imekuwa na mtindo wa kuzindua simu zenye muonekano mmoja lakini zikiwa na majina tofauti baina ya nchi na nchi, kama ilivyo Tecno Camon iClick 2 ambayo kwa barani Afrika ni Tecno Camon 11.
Kwa mujibu wa tovuti hiyo, Tecno Camon i4 yenyewe inakuja na kamera tatu zenye uwezo wa Megapixel 13, Megapixel 8 na Megapixel 2, kwa mbele inakuja na kamera moja ya Selfie yenye uwezo wa Megapixel 16 yenye uwezo wa kurekodi video za 1080p@30.
Mbali na kamera simu hii inasemekana kuja kwa matoleo matatu, toleo moja likiwa na RAM ya GB 2, toleo jingine GB 3 na toleo la mwisho likiwa na GB 4. Vilevile simu hizi zitakuwa na ukubwa wa ROM wa kuchagua kati ya GB 32 na GB 64. Kwa upande wa processor simu hii inakuja na processor ya MediaTek Helio A22 yenye uwezo wa Quad core 2 GHz Cortex A53.
Simu hii mpya Tecno Camon i4, ambayo itakuja Afrika kwa jina lingine, inategemea kuja na battery ya Li-Po yenye uwezo wa 3500 mAh yenye uwezo wa kudumu na chaji siku moja kulingana na matumizi yako. Kwa upande wa bei simu hii nchini india inauzwa rupee Rs 9,499 kwa toleo lenye GB 32 ambayo ni sawa na Tsh 319,000 bila kodi. Kwa toleo la GB 64 inauzwa rupee Rs 11,999 ambayo ni sawa na Tsh 402,000 bila kodi, kumbuka bei hizi zinaweza kubadilika kwa Tanzania.
Kwa sasa bado haijajulikana jina ambalo litatumika kwenye simu hii itakapokuja hapa Afrika (Labda Tecno Camon 12), hivyo endelea kutembelea Tanzania Tech tutakujuza pindi simu hii itakapo fika hapa nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla.