Kampuni inayo jihusisha na utoaji wa huduma za usafirishaji ya Taxify, hivi karibuni imetangaza kubadilisha jina lake pamoja na nembo yake ya biashara na kuwa Bolt.
Hata hivyo inasemekana kuwa mabadiliko hayo yanatokana na malengo mapya ya kampuni hiyo katika biashara ya usafirishaji. Taxify au Bolt kwa sasa inatoa huduma zake kwenye nchi zaidi ya tano barani ya Afrika, huku ikiwa na muda wa miaka mitano toka ilipo anzishwa.
Kwa mujibu wa tovuti ya Mwananchi, Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi mwenza wa Bolt, Markus Villig amesema jina hilo la Bolt litaanza kufahamika hatua kwa hatua katika masoko ya kimataifa katika wiki zijazo.
Hata hivyo wateja na watumiaji wa huduma na app ya Taxify, hawana haja ya kufanya chochote zaidi ya kufanya update za app hiyo pale itakapo tangazwa. Kwa sasa huduma zote zinaendelea kama kawaida hivyo wateja wa huduma hizo hawana haya ya kuwa na wasiwasi wowote kuhusu mabadiliko hayo.
Naye Meneja Mkazi wa Bolt nchini Tanzania, Remmy Aseka alisema bidhaa ya kwanza ya kampuni hiyo ya usafirishaji ilikuwa ni kutoa suluhisho na kurahisisha upatikanaji wa huduma za teksi kwa wateja wake lakini watu wategemee kupata urahisi zaidi kupitia Bolt.