Mpaka sasa na hakika utakuwa unaijua Roboti Sophia, kama hujui hii ni Roboti ya kwanza kabisa iliyopewa Uraia wa Saudi Arabia, mbali na kupewa uraia Roboti hii inauwezo wa kufanya mambo mbalimbali ikiwa pamoja na kuonyesha hisia kwa uso pamoja na kuzungumza na binadamu kwa kutumia mfumo wa AI au Artificial Intelligence.
Sasa hivi karibuni roboti sophia kwa mara ya kwanza anatarajiwa kuja Afrika kwenye mkutano wa Egypt’s Creative Industry Summit unaotegemewa kufanyika kuanzia tarehe 17 mwezi huu wa nne mpaka tarehe 18 huko nchini Misri.
Hata hivyo Mkutano huo unalenga maendeleo ya hivi karibuni katika maeneo ya matangazo, masoko na ubunifu nchini Misri na kwa upande wa nchi za Kiarabu Roboti sophia anategemewa kuwa kwenye mkutano huo kuongelea maswala hayo.
Hivi karibuni Roboti Sophia amekuwa akionekana sehemu nyingi mbalimbali huku siku za karibuni, roboti huyo alionekana akiongea na muigizaji maarufu na mwanamuziki wa zamani Will Smith, ambapo Will Smith alipata nafasi ya kuongea na roboti hiyo pamoja na kujua hisia zake za kimapenzi.
Sophia ni roboti ambayo iko mithili ya binadamu ambayo imetengenezwa na kampuni maarufu ya utengenezaji wa roboti ya Hanson Robotics. Kampuni yenye makao yake makuu huko Hong Kong na ni moja kati ya kampuni inayo julikana sana kwa utengenezaji wa roboti mbalimbali kama binadamu maarufu kama (humanoid robot).