Kukiwa tayari na kiasi kikubwa cha taarifa zinazofahamika juu ya toleo linalokuja la simu toka kampuni ya Google, Google wameweka wazi siku ambayo simu hizo za Pixel 8 zitatangazwa rasmi.
Jumatano ya Tarehe 4 Oktoba ndipo ambapo Google watazindua rasmi simu zao za Pixel 8 na Pixel 8 Pro zikiwa ni mwendelezo wa matoleo ya simu zao za hadhi ya juu (Flagship) na toleo la tatu tangu Google kuanza kutumia chipset yao binafsi (Google Tensor).
Katika tukio hilo, tunatarajia Google kutangaza mabadiliko na maboresho waliyoyafanya katika toleo hilo, baadhi ambayo tayari yanafahamika kutokea katika tetesi mbalimbali. Tunategemea kuboreshwa kwa Kamera, Umbo la Simu kuwa lenye kona za uduara zaidi (Rounded Edges), Chipset mpya ya Google Tensor G3 ambayo inategemewa kuleta maboresho makubwa katika kasi ya simu pamoja na utunzaji wa chaji, pamoja na mabadiliko mengine kadha wa kadha.
Google wamezoeleka kuzindua simu zao mpya za hadhi ya juu mnamo robo ya mwisho ya mwaka, na hii itakuwa ni mwendelezo katika tamaduni hiyo, ikiwa ni mara tu baada ya Apple kuzindua simu zao za iPhone mwezi Septemba.
Tunatarajia pia kuzinduliwa kwa bidhaa nyingine kama saa janja, ikiwezekana pia na earbuds mpya kutoka kwao. Yote yatafahamika kwa undani zaidi siku husika. Tembelea makala zetu zaidi kujua tetesi na taarifa juu ya ujio wa bidhaa kutoka kwa makampuni mbalimbali mwisho huu wa mwaka.