Hatimaye kampuni ya Samsung hivi leo imetambulisha toleo jipya la simu zake za daraja la kati simu ya Galaxy M51. Simu hii ni moja kati ya simu ambazo zinakuja na battery kubwa pengine kuliko simu nyingi za daraja la kati kutoka Samsung.
Kwa kuanza simu hii inakuja na kioo cha inch 6.7 huku kikiwa kimetengenezwa kwa teknolojia ya Super AMOLED. Kwa juu ya kioo hicho, Galaxy M51 inakuja na kamera ya mbele yenye uwezo wa Megapixel 32 huku ikiwa na uwezo wa kuchukua video za hadi pixel 1080p@30fps.
Kwa nyuma, Galaxy M51 inakuja na kamera nne, kamera kuu ikiwa na uwezo wa Megapixel 64 huku nyingine ikiwa na uwezo wa Megapixel 12 na mbili za mwisho zikiwa na uwezo wa Megapixel 5 kila moja. Kamera hizo zote zinakuja na uwezo wa kuchukua video za hadi 4K.
Kwa upande wa sifa za ndani, Galaxy M51 inakuja na RAM ya GB 6 huku ikisaidiwa na uhifadhi wa ndani wa hadi GB 128 huku ikiwa na uwezo wa kuongezewa na Memory card ya hadi GB 512. Mbali na hayo, simu hii inaendeshwa na processor ya Qualcomm Snapdragon 730, yenye uwezo wa CPU ya hadi Octa-core 2×2.2 GHz Kryo 470 Gold & 6×1.8 GHz Kryo 470 Silver.
Tukija kwenye upande wa Battery, Galaxy M51 inakuja na battery kubwa ya 7000 mAh, battery hii ni moja kati ya battery kubwa kuwepo kwenye simu za Samsung za daraja la kati. Battery hiyo pia inakuja na teknolojia ya Fast Charging (25w), ambayo inafanya simu hii kujaa chaji kwa haraka.
Kwa upande wa bei, kwa sasa Galaxy M51 imezinduliwa huko nchini Ujerumani huku ikitarajiwa kuingia sokoni rasmi siku ya tarehe 11 mwezi wa tisa mwaka 2020. Kwa mujibu wa Price in Tanzania, Samsung Galaxy M51 inatarajiwa kuuzwa hapa Tanzania kwa takribani TZS 1,100,000 pamoja na kodi. Kumbuka bei inaweza kubadilika pale simu hii itakapoingia sokoni hapa Tanzania.