Ni wazi kuwa watu wengi siku hizi wamekuwa wakitumia muda mwingi wa ziada kutizama video au kujifunza mambo mbalimbali kupitia video kwenye mtandao wa YouTube, pengine hii ndio sababu ya Youtube kuwezesha sehemu ya kuchat kwenye mtandao huo. Hapo mwanzoni sehemu hii ya kuchat ilikuwa inapatikana kwenye programu za Youtube za iOS na Android pekee na sasa sehemu hii inakuja rasmi kwenye tovuti ya YouTube.
Kwa mujibu wa tovuti mbalimbali, sehemu hiyo mpya itakuja kwenye tovuti ya mtandao huo na itakuwa inaonekana kwa wale wanaotumia kompyuta na kwa wale wanaotumia simu wataweza kuendelea kutumia sehemu hiyo kupitia kwenye programu za YouTube za Android na iOS. Kama bado ujajua jinsi ya kuchat ndani ya mtandao wa YouTube kwa kutumia programu za Android na iOS unaweza kujifunza hatua kwa hatua hapa.
Kwa watumiaji wa kompyuta sehemu hiyo inategemewa kuwepo upande wa kulia juu karibia na kitufe cha ujumbe wa taarifa (Notification). Kwa bofya hapo utaweza kufungua ukurasa juu ya ukurasa uliopo kwenye mtandao wa YouTube na utaweza kuanza kuchat na watu mbalimbali au kushiriki (share) nao video moja kwa moja kuptia sehemu hiyo.
Hata hivyo kwa sasa bado watu wengi hawajapata sehemu hii hivyo endelea kusubiri uenda siku za karibuni utaweza kuona sehemu hii kwenye tovuti ya YouTube kupitia kompyuta yako. Kama unatumia Android au iOS unaweza kujifunza hatua kwa hatua jinsi ya kutumia sehemu hii kwenye simu yako kwa kubofya link hapo juu.