Msanii maarufu anaetokea nchini Senegal, Akon hivi karibuni ametangaza kuzindua sarafu yake ya kidigital inayoitwa AKoin. Msanii huyo amesema ana amini sarafu hiyo inaweza kusaidia bara la Afrika kwa miaka ya karibuni. Kwa mujibu wa tovuti ya BBC, akon alisema hayo kupitia tamasha la Cannes Lions siku ya Jumatatu mwezi huu..
Mbali na hayo, Akon anasema kuwa anapanga kujenga mji wa kidijitali nchini Senegal utakao kuwa ndio unatumia sarafu hiyo ya kidigital ya AKoin. Hata hivyo kupitia tovuti ya sarafu hiyo ya AKoin, mji huo utajengwa nchini Senegal dakika chache kutoka eneo la uwanja wa ndege wa kimataifa, kilometa chache kutoka mji mkuu wa Senegal Dakar, kwenye eneo la ukubwa wa ekari 2,000 ambalo msanii huyo alipewa na raisi wa Senegal kwaajili ya kufanya shughuli hiyo.
Kwenye tovuti hiyo ya AKoin, mji huo unaotarajiwa kujengwa na Msanii Akon, umeelezewa kuwa kama vile ni mji wa Wakanda, mji wa kusadikika ulio onekanoa kwa mara ya kwanza kwenye filamu ya Black Panther iliyotoka mapema mwaka huu 2018.
“Chini ya mazingira ya sarafu ya kidijitali ya AKoin, wateja wataweza kununua, kuhifadhi na kutumia sarafu hiyo moja kwa moja kutoka kwenye simu zao za mkononi. Inarudisha uwezo kwa raia na kurudisha usalama katika mazingira ya sarafu hiyo”, Akon alielezea.
”Pia inawaruhusu watu kuitumia kwa njia ambayo wanaweza kujiendeleza na kutoruhusu serikali kufanya mambo yanayokwamisha maendeleo, “Nilikuja na mradi huu hivyobasi nataka magwiji kuketi chini na kuona utakavyofanyika”, alisema msanii huyo maarufu wa senegal anaeishi nchini marekani.
Kwa wale ambao hamjui sarafu ya kidigital, hii ni aina ya sarafu kama vile Bitcoin ambayo kwa lugha ya kigeni inaitwa Cryptocurrency, hii ni fedha ya kidijitali inayofanya operesheni huru kando na benki kuu. Sarafu ya kwanza ya kidijitali ni Bitcoin ambayo ilianzishwa na mtu asiyejulikana kwa jina Satoshi Nakamoto mwaka 2009. Unaweza kusoma HAPA kujua zaidi kuhusu Bitcoin.
Hata hivyo Akon amekiri kwamba hajui maswala ya kiufundi ya uwekezaji huo mpya. hivyo anategemea kupata usaidizi kutoka kwa wataalamu wa maswala hayo. Akon amekuwa akisaidia Afrika kupitia shirika lake la Akon Lighting Africa, ambayo husaidia kufunga (solar) au umeme wa nishati ya jua sehemu zisizokuwa na umeme barani Afrika. Shirika hilo limepewa kipaumbele na kutambulika na Umoja wa mataifa kutokana na msaada anaowezesha msanii huyo.