Wakati Tanzania ikiwa bado ina jikongoja kwenye huduma za malipo ya mtandaoni, Nchini Afrika ya Kusini mambo yanaendelea kuwa mazuri kwani hivi karibuni wananchi wa nchini humo wataweza kufurahia huduma mpya za malipo za Samsung Pay.
Kama ulikuwa hujui kuhusu Samsung Pay, hii ni huduma itakayo kuwezesha kuweza kufanya malipo kwa kutumia simu yako ya mkononi, Yaani utaweza kunakili kadi zako za benki na kuzihifadhi kwenye simu yako ya Samsung na utaweza kufanya malipo kwa kusogeza simu yako karibu na mashine maalum ya kulipia na utaweza kudhibitisha kwa kutumia fingerprint ya simu yako na utaweza kufanya malipo moja kwa moja.
Kwa mujibu wa tovuti ya Samsung kupitia mkurugenzi mtendaji wa Samsung Electronics kwa Afrika Sung Yoon huduma hiyo inategemewa kuzinduliwa rasmi mwezi wa sita na inategemewa kuanza kutumika kuanzia mwezi wa Saba. Hata hivyo Samsung imekuwa ikipanua huduma hii ya malipo kwani siku za karibuni Samsung ilizindua huduma hizo nchini italia na kuruhusu wakazi wa nchini humo kufanya malipo kwa mfumo huo.
Kwa hapa Afrika ni wazi kuwa, Afika ya kusini ni moja kati ya nchi inayo kuwa haraka sana kiteknolojia kwani makampuni mengi yenye kutoa huduma mbalimbali za teknolojia duniani yamekua na matawi ya makampuni yao nchini humo huku kampuni nyingine nyingi kama Spotify zikiendelea kufungua matawi ya kampuni zake nchini humo.
Kuhusu uwezekano wa huduma hii kuja Tanzania ni wazi kuwa jambo hilo litakuwa ni la kusubiri kwa muda mrefu kwani hata watumiaji wa kadi za benki kufanya malipo bado hawapo wengi nchini hivyo hadi hapo watumiaji wa huduma hizo watakapo ongezeka ni vyema kuendelea na shughuli zingine kwanza.