Samsung inategemea kuzindua simu yake mpya ya Samsung Galaxy Note 9 tarehe 9 ya mwezi ujao mwaka huu 2018, wakati zikiwa zimebaki wiki chache hadi kuzinduliwa kwa simu hii tayari kumesha vuja picha zenye muonekano halisi wa simu hiyo mpya.
Picha hizi ambazo zinaonyesha muonekano halisi wa simu hii zinaonyesha Galaxy Note 9 itakuja na mtindo kama wa Galaxy Note 8, huku mabadiliko makubwa ya muonekano yakiwa nyuma ya simu hii ambapo sehemu ya fingerprint sasa inaonekana ikiwa chini ya kamera hizo, tofauti na toleo la Galaxy Note 8 ambayo sehemu hiyo iko pembeni ya kamera.
Kuthibitisha kwamba huu ndio muonekano wa Galaxy Note 9, picha hizi zinafanana na picha za muonekano wa simu hii zilizovuja wiki kadhaa zilizopita, Ukichangia na picha iliyosambaa sana wiki hii ambayo inaonyesha mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Samsung akitumia simu hiyo ambayo pia ina muonekano wa nyuma ambao ni sawa na kwenye picha hizi.
Kwa upande wa sifa za simu hii, kama tulivyo angalia kwenye makala iliyopita, sifa zinazotegemewa ni pamoja na kalamu ya simu hiyo ambayo sasa inakuja na uwezo wa kutumia teknolojia ya Bluetooth, ambayo itamruhusu mtumiaji kuweza kutumia kalamu hiyo kuendesha mambo mbalimbali kwenye simu hiyo kama kuwasha muziki na kupeleka nyimbo mbele na nyuma pamoja na mambo mengine.
Mbali na hayo Galaxy Note 9 inatarajiwa kuja na maboresho zaidi ya mfumo wake wa uendeshaji na kamera ambazo zinasemekana kuwekewa teknolojia mpya ya kuweza kupiga picha vizuri hasa kwenye mwanga mdogo au wakati wa usiku.