Hivi karibuni kampuni ya Oppo imeonyesha aina mpya ya kioo ambacho kinawezekana kutumika kwenye simu zake mpya za hivi karibuni, kioo hicho ambacho kinaonekana kujikunja kwa zaidi ya nyuzi 88 kimepewa jina la “Waterfall Screen”.
Kioo hicho kimejikunja kwa asilimia kubwa tofauti na vioo vya Curved display ambavyo tayari tumesha viona kwenye simu mbalimbali kama Galaxy S7 Edge na nyingine. Hata hivyo kioo hicho kimeongezewa teknolojia zaidi ambapo mtu akiwa anatumia simu yenye kioo hicho inaonekana kama simu hiyo haina pembe za pembeni kabisa huku ikiwa na kioo kirefu zaidi.
Mbali ya muonekano huo, Oppo pia imewezesha teknolojia ya kiasasa ambapo sehemu zilizo jikunja kwenye simu hio zinafanya kazi huku picha zikionekana kuanzia kwenye pembe moja na kupotelea kwenye pembe nyingine kama maporomoko ya maji au waterfall.
Hata hivyo teknolojia hiyo ya kioo inafanya simu zitakazokuwa na kioo hicho kutokuwa na vibonyezo vya pembeni ambavyo mara nyingi hutumika kuongeza na kupunguza sauti pamoja na kitufe cha kuwasha ambacho mara nyingi huwa kwa upande wa pili.
Kwa sasa bado hakuna ripoti simu gani ya Oppo itakuwa na kioo hiki, japo kwa mujibu wa tovuti ya The Verge inasemekana kuwa pengine simu mpya inayokuja kutoka kampuni hiyo ndio itakayo kuwa na teknolojia hiyo mpya ya kioo.
Picha hapo juu inaonyesha simu mpya yenye kioo cha Waterfall Screen (Kulia) ikilinganishwa na simu ya Oppo Find X yenye kioo cha kujikunja cha kawaida.
Kupata taarifa zaidi kuhusu simu hii pamoja na ujio wa kioo hicho hakikisha unaendelea kutembelea tovuti ya Tanzania Tech kila siku, bila shaka tutakuwa wakwanza kukujilisha kuhusu hili.