Kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo urahisi wa kufanya manunuzi mtandao unapozidi kuwepo hasa hapa kwetu Tanzania, Siku za karibuni tulisikia Vodacom Tanzania ikija na huduma ya M-Pesa Mastercard huduma ambayo inakusaidia kuweza kufanya manunuzi kupitia Mastercard ambayo unaweza kutengeneza kupitia huduma ya M-Pesa.
Sasa hapo mwaka jana 2018 kampuni ya kutoa huduma za simu ya Tigo Tanzania, ilikuja na huduma mpya ambayo inaruhusu wateja wake kuweza kununua apps mbalimbali kupitia soko la Play Store kwa kutumia Tigo Pesa.
Kwa sasa huduma hiyo tayari inatumiawa na watu wote na unaweza kuanza kutumia huduma hii kwa kuingia kwenye soko la Play Store na bofya sehemu ya manunuzi kwenye apps, muziki au movie kisha utaona sehemu mpya ya Lipia kwa Tigo Pesa (Use Tigo Pesa billing). Kama unatumia simu yenye Laini mbili hakikisha laini ya Tigo ndio iliyopo kwenye sehemu ya kupiga simu na kupokea SMS, pia ili kuondokana na matatizo au kuchelewa kwa malipo ni vizuri kutumia Internet ya Tigo japo kuwa sio lazima.
Vodacom Tanzania nayo pia inayo huduma kama hii ambayo pia inawezesha wateja wake kuweza nunua apps mbalimbali kupitia Play Store kwa kutumia salio la kawaida. Huduma hiyo kwa sasa inapatikana pale utakapo kuwa unatumia Internet ya mtandao wa Vodacom, kama unatumia WiFi au mtandao mwingine kwenye simu yako unaweza usione sehemu hii hata kama laina ya Vodacom iko kwenye simu yako.
Kwa habari zaidi za teknolojia na kuelewa zaidi kuhusu njia mpya za kufanya manunuzi mtandaoni hakikisha unaendelea kutembelea Tanzania Tech kila siku, pia tembelea sehemu ya Pesa mtandaoni kupata taarifa zaidi juu ya kufanya manunuzi mtandaoni.