Kwa wale ambao ni watumiaji wa tovuti ya barua pepe ya Gmail hivi karibuni wategemee kuona muonekano mpya, kwani inasemekana Google inategemea kufanya maboresho makubwa ya tovuti hiyo ikiwa pamoja na kuwekea muonekano kabisa tovuti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti za baadhi ya wateja wa kulipia wa G-suite, Google ilituma barua pepe za kuwajulisha wateja wake hao kuhusu mabadiliko hayo ambayo yana tegemewa kuja kwa watumiaji wa tovuti ya Gmail kwenye siku za karibuni. Hata hivyo inasemekana kuwa Google imeanza kuruhusu baadhi ya wateja wake wa G-Suite kujaribu muonekano huo ambao unasemekana kuwa ni muonekano bora zaidi.
Katika muonekano huo mpya, Google inasemekana kuleta sehemu mpya ya Reply ambayo itakuwa inafanya kazi kama ilivyo ile App au programu ya Reply kutoka Google. Sehemu hiyo mpya itakuwezesha kujibu barua pepe zako kwa kutumia mfumo wa AI au Artificial Intelligence, kama vile jinsi programu hiyo ya Android ya Reply inavyo fanya kazi.
Hapo chini ni picha ya muonekano mpya wa tovuti hiyo ya barua pepe ya Gmail pamoja na sehemu hiyo ya Reply iliyo zungushiwa rangi nyekundu chini ya picha hiyo.
Mbali na hayo, Sehemu nyingine inayotegemewa kufanyiwa mabadiliko ni pamoja na njia za kuchagua muonekano wa barua pepe zako ndani ya ukurasa wa Inbox. Muonekano huo mpya utakuja na sehemu mpya ambayo zitakuwezesha kuchagua aina ya muonekano unayotaka kulingana na wingi au uchache wa barua pepe zako ndani ya ukurasa wa inbox kwenye tovuti hiyo ya barua pepe ya Gmail.
Kama inavyo onekana hapo juu, kutakua na aina mpya tatu za muonekano ambazo utaweza kuchagua. Kutakuwa na aina ya kwanza ambayo ni Default, aina hii itakupa uwezo wa kuona vitu kama aina za viambatanisho (attachment) vilivyoko kwenye barua pepe kabla ya kuifungua, ikiwa pamoja na picha, slides, nyaraka (documents) pamoja na majedwali au (spreadsheets).
Aina nyingine itakuwa ni Comfortable, aina hii itakuwezesha kuondoa nembo zote zinazo onyesha aina za viambatanisho (attachment) na badala yake itabakiza pini maalumu inayotumika sasa kuonyesha kwamba barua pepe inakuja na kiambatanisho au (attachment).
Aina ya mwisho ya tatu itakuwa ni Compact, aina hii inafanana kabisa na aina ya pili ambayo ni Comfortable lakini utofauti wa aina hii upo kwenye mpangilio kwani aina hii itapunguza ukubwa wa urefu kutoka barua pepe moja hadi nyingine kwenye ukurasa wa inbox ndani ya tovuti hiyo ya barua pepe ya Gmail.
Kwa sasa bado haijajulikana ni lini muonekano huo mpya utawafikia watumiaji wa tovuti hiyo ya barua pepe ya Gmail, lakini kama wewe unatumia barua pepe ya Gmail kwa kutumia kompyuta, tegemea kuona muonekano huo mpya siku za karibuni.