Linapokuja swala la kununua TV bora yenye teknolojia ya 4K ni wazi kuwa kila mtu anachaguo lake kutokana na aina ya TV ambayo nafsi yake inapendelea. Lakini pia tukija kwenye upande mwingine ni ukweli kuwa, watu wengi hasa hapa Tanzania huangalia baadhi ya vitu kama vile ukubwa wa TV na muonekano wa picha na kusahau mambo mengine mengi ya muhimu.
Kwenye makala hii ya leo nitaenda kuongelea kidogo hatua za kufuata pale unapochukua uamuzi wa kwenda kununua TV mpya ya 4K, kumbuka ni muhimu kusoma makala hii yote ili kujua mambo yote kwani na uhakika itakusaidia kwa namna moja ama nyingine. Basi bila kupoteza muda twende tuka angalie mambo haya.
1. Viunganishi
Ni wazi kuwa mara nyingi watu wanapo kwenda kununua TV wanasahau kuangalia viunganishi kama vile USB, HDMI, HDCP na Vinginevyo. Hivi ni viunganishi vya muhimu sana kwani unapo nunua TV hasa ya 4K unahitaji idumu kwa muda mrefu na kwa sababu teknolojia inakuwa kwa kasi sana unaweza kudhani huitaji yote hayo kwa sasa, lakini kutokana na teknolojia unaweza kujikuta siku umenunua kifaa ambacho kinatumia moja ya viunganishi hivyo na unashindwa kukitumia kutokana na TV yako kukosa aina fulani ya kiunganishi. Hivyo basi, ni muhimu kuangalia TV yenye viunganishi vingi vya ziada kwani huwezi kujua ni muda gani unaweza kuhitaji viungani hivyo.
Kumbuka kuwa ni vyema kuhakikisha TV yako inakuja na viunganishi vya USB yenye kucheza audio na video za format zote, Pia sehemu za HDMI pamoja na sehemu ya headphone jack au Aux kwaajili ya sauti.
2. Fahamu TV yenyewe Kwanza
Sio watu wote wenye tabia ya kuchunguza bidhaa kabla ya kununua, lakini wewe msomaji wa Tanzania Tech napenda kukushauri kuwa hata kama unaijua TV unayotaka kununua ni vyema kuchukua muda wako wa ziada kufanya uchunguzi kwani unaweza kugundua mambo mengi ambayo ulikuwa huyajui hapo awali. Kwa sasa mtandao kama YouTube unasaidia sana, unaweza kuingia kwenye mtandao huo kisha kutafuta video zenye kuonyesha njia za kutambua 4K TV feki na 4K TV halisi, kulingana na aina ya kampuni ya TV unayotaka kununua.
Mbali na hayo ni vyema kujua sifa za TV ya 4K unayotaka, hii itakusaidia kuweza kujua kama TV hiyo itakidhi haja za macho yako. Nakushauri tumia kati ya siku 3 hadi wiki moja kuweza kufahamu vizuri aina ya TV unayohitaji hata kama ulikuwa unaijua kabla ya hapo.
3. Fahamu Kuhusu LED, LCD na OLED
Kabla ya kununua TV yenye 4K ni vyema ujue kwanza aina hizi za teknolojia ya Vioo, aina hizi ndio zitaweza kukusaidia kuweza kufanya uamizi mzuri na sahihi wa kununua TV bora ya 4K na ya kisasa zaidi inayo lingana na thamani ya pesa zako. Ushauri wangu ni kuwa kama unataka TV nzuri yenye 4K basi ni vyema kuchagua TV yenye kioo cha OLED.
4. Hakikisha Ina Uwezo wa HDR
Unapotaka kununua TV hasa yenye 4K ni muhimu sana sana sana kuhakikisha inauwezo wa teknolojia ya HDR. Muuzaji anaweza kukwambia TV nyingi za 4K tayari zinayo HDR lakini sio kweli sio kila TV yenye 4K basi inayo teknolojia ya HDR. Hakikisha kwenye box au kitabu cha TV yako imeandikwa HDR kwani teknolojia hii itakupa uwezo mzuri zaidi wa kuangalia TV yako huku ikionyesha rangi vizuri zaidi na mwanga mzuri.
5. Muundao wa TV
Kama unataka kununua TV ya 4K ni vyema kuangalia muundo wa TV kwani kuna wakati unakuta mtu anakimbilia kununua TV ya 4K iliyojikunja (Curved) kwa sababu ya muonekano wake mzuri. Lakini naomba nikushauri kuwa, mara nyingi TV zilizo jikunja (Curved) hizi ni nzuri kwa kuangalia watu wengi na kama TV yako umepanga kuwa TV ya familia au ya kwako binafsi nakushauri ununue TV ya muundo wa kawaida na sio iliyojikunja.
Na hayo ndio mambo ya muhimu ya kufuata kabla ya kununua TV ya 4K, kama unataka kujua mambo mengine unaweza kusoma makala hii hapa na utaweza kujua mambo mengine ya muhimu ya kufuata. Mambo hayo yanaweza kutumiwa kwa yoyote anaetaka kununua TV ya aina yoyote iwe 4K au TV ya kawaida.
Maoni Nawapongeza kwa mambo mbalimbali mnayo tufundisha
Tunaomba mngetuchambulia na technolojia ya qled,uled na o led,au mtuwekee tv bora kwa mwaka 2019 au 2020