Hapo asubuhi ya jana, kampuni ya Facebook kupitia ukurasa wake wa habari ilichapisha taarifa juu ya udukuwaji uliofanyika siku za karibuni. Kupitia habari hiyo Facebook imeandika kuwa imegundua tatizo kwenye mtandao huo ambalo limeletwa na mdukuaji au wadukuaji ambapo akaunti zaidi ya milioni 50 zinaweza zikawa zimeadhiriwa.
Kwa mujibu wa Facebook kupitia udukuaji huo ulifanyika kwa kutumia sehemu maalum inayopatikana kwenye App ya Facebook ambayo inajulikana kama “View As”. Kwa wale ambao hamjawahi kutumia sehemu hii, hii ni sehemu inayo kuruhusu kuweza kuangalia ukurasa wako kama mtu mwingine ili kuweza kuona ukurasa wako unaonekanaje pale mtu anapokuwa ana tembelea ukurasa huo.
Sasa kupitia udukuaji uliofanyika Facebook inadai kuwa, wadukuaji au mdukuaji anaehusika alikuwa akitumia sehemu hiyo kuweza kuiba token (ziko kama mfululizo wa namba nyingi) ambazo hizi ndio husaidia mtu anapokuwa ameingia (login) kwenye App ya mtandao huo kuweza kuendelea kutumia mtandao huo bila kuingia (login) kila wakati anapotaka kutumia app hiyo ya Facebook.
Hata hivyo makala hiyo inaendelea kuandika kuwa, kampuni ya Facebook iligundua kuhusu udukuaji huo siku ya tarehe 25 ya mwezi September baada ya kupewa taarifa na Guy Rosen ambaye ni Makamu wa rais wa usimamizi wa bidhaa wa kampuni ya Facebook. Hata hivyo mara baada ya kupewa taarifa na mfanyakazi huyo, Facebook ilichukua hatua ya kuzima sehemu “View As” na baadae kulazimisha watumiaji milioni 90 walio wahi kutumia sehemu hiyo kwa kipindi kirefu kuweza kuingia (Login) upya kwenye akaunti zao na kuwapa ujumbe wenye kuonyesha ni kwanini.
Kwa mujibu wa tovuti ya TheVerge, udukuaji huu unakuja masaa machache kutoka mdukuaji salama “white hat hacker” wa nchini Taiwan Chang Chi-yuan, kutangaza kuwa amegundua tatizo kwenye mtandao wa Facebook tatizo ambalo linamuezesha kuweza kufuta ukurasa wa Facebook wa mkurugenzi mtendaji wa Facebook Mark Zuckerberg. Hata hivyo mdukuaji huyo salama alitanga hayo kupitia kwenye mtandao wa Facebook na kusema kuwa ataonyesha tukio hilo mubashara kupitia ukurasa wake wa Facebook kama kitendo cha kufundisha watu jinsi ya kugundua matatizo kama hayo.
Hata hivyo baadae “white hat hacker” huyo alitangaza kuwa ameamua kuwasilisha tatizo hilo kwa kampuni ya Facebook na hivyo hatoweza kuonyesha mubashara tukio hilo la kifuta ukurasa wa Zuckerberg na kudai kuwa atakuja kuonyesha pale atakapo pewa zawadi ya pesa za kugundua tatizo hilo kwenye mtandao huo. Facebook na makampuni mengine makubwa ya mtandaoni huwa na utaratibu wa kutoa zawadi ya pesa kwa wadukuaji salama “white hat hacker” wakionyesha matatizo mbalimbali ya ulinzi ya mitandao yao.
Kama ilivyo andikwa kwenye ukurasa wake, Facebook hutoa kiasi cha chini cha dollar za marekani $500 ambayo ni sawa na Tsh 1,143,000 kwa tatizo la ulinzi litakalo gundulika na mdukuaji salama na hutoa pesa zaidi ya hizo kulingana na tatizo lilogundulika, yaani ni sawa na kusema tatizo linapokuwa kubwa zaidi basi ndio kiasi cha pesa kinakuwa kikubwa zaidi.
Mdukuaji huyo ChiYuan Chang, anajulikana kwa kazi yake ya udukuaji salama na ameandikwa kwenye ukurasa wa mtandao wa LINE wa mwaka 2016 kama mmoja wa wadukuaji wazuri waliosaidia mtandao huo kugundua matatizo mbalimbali.
Kwa sasa Facebook imeshatoa taarifa kwa mamlaka husika nchini marekani na tayari sehemu hiyo imeshafanyiwa marekebisho ila Facebook inasema kuwa bado haijampata anae husika na udukuaji huo na inawezekana kutokumjua kabisa kutokana na aina ya udukuaji uliofanyika. Vilevile Facebook hivi leo inakabiliwa na kesi ya kujibu iliyofunguliwa na baadhi ya watumiaji wa mtandao huo wakidai kuwa udukuaji huo wa Facebook umesababisha uwezekano wa watu kuweza kuiba utambulisho wao “identity theft” kwa urahisi zaidi.
huu ujumbe nami niliupata juzi baada ya kuingia kwenye acount yangu ya facebook kupitia laptop so iliniomba niingie tena upya.