Mpaka sasa na uhakika kwa namna moja ama nyingine umeshasikia kuhusu mtandao wa 5G, kama bado hujasikia kuhusu mtandao huu basi ni wazi umeshasikia kuhusu mtandao wa 4G. Kama tayari unajua kidogo kuhusu 4G basi 5G ni toleo jipya la 4G yaani hii maana yake ni fifth generation au kwa kiswahili kizazi cha tano cha mtandao wa simu.
Sasa leo hapa Tanzania Tech tutaenda kukujuza kidogo kuhusu mtandao wa 5G pamoja na kujua 5G imetokea wapi na mengine mengi.. basi bila kupoteza muda let’s Jump right in..
5G ni nini ?
Kwa kuanza kama nilivyokwambia hapo awali, 5G ni kizazi cha tano cha mtandao wa simu, mtandao huu wa kizazi cha tano unategemewa kuwa ni wa kasi zaidi kuliko 4G, mtandao wa 5G unategemewa kuanza kufanya kazi duniani kuanzia mwaka 2020 huku ukishirikiana na mitandao ya 3G pamoja na 4G.
Mtandao wa 5G Utakuwa na Kasi Gani ?
Kwa sababu bado mtandao huu uko kwenye hatua za matengenezo hadi sasa bado hakuna majibu kamili kuhusu kasi ya Mtandao wa 5G, ila kwa mujibu wa vigezo vilivyo tolewa na GSMA mtandao wa 5G unatakiwa kuwa na kiwango cha chini cha Speed ya kudownload hadi GB 1 kwa sekunde. Hata hivyo watu wengi wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusu kasi ya mtandao huo huku wengine wakisema mtandao huo utakuwa na speed ya kudownload hadi GB 10 kwa sekunde, huku wengine wakidai mtandao huo utakuwa na kasi zaidi hadi GB 800 kwa sekunde.
Kwa sasa bado hakuna kiwango kamili cha kasi ya 5G kinacho julikana au kilicho tangazwa, ila kwa mujibu wa GSMA ni lazima mtandao wa 5G uwe na kasi ya kudownload angalau GB 1 kwa sekunde.
Mtandao wa 5G Unategenezwa na Nani ?
Kwa sasa kwa mujibu wa mtandao wa wikipedia, kazi ya kuunda miundombinu itakayo wezesha mtandao wa 5G inafanywa na kampuni mbalimbali ikiwa pamoja na kampuni za Intel, Qualcomm, Lenovo, Nokia, Huawei, Ericsson, ZTE pamoja na Samsung.
Pia zipo kampuni mbalimbali zinazoshirikiana na hizi kuwezesha teknolojia hii hivyo hizo hapo juu ni baadhi tu ya kampuni hizo zinazo tambulika au zenye majina makubwa.
Je Utaweza Kutumia 5G Kwenye Simu Yako ?
Kama nilivyo sema hapo awali 5G inategemewa kuzinduliwa rasmi mwaka 2020, hadi muda huo simu ambazo zitakuwa hazina uwezo wa 5G hazitakuwa na uwezo wa kutumia mtandao huo bali ni imani yangu hadi kufika mwaka huo tutakuwa tumesha ona simu nyingi mpya ambazo zitakuja na teknolojia hiyo mpya. Vilevile kutumia teknolojia ya 5G kutategemeana na mtandao wa simu unaotumia kama utakuwa umeshafunga mitambo yenye uwezo wa kufikisha teknolojia hiyo kwa watumiaji wake.
Hata hivyo teknolojia ya 5G haitakuja kuondoa teknolojia ya 4G, kwani ni wazi kuwa teknolojia ya 5G itatumia muda mrefu sana kusambaa duniani kote hivyo ni wazi bado nchi nyingine duniani zitakuwa hazina uwezo wa kutumia 5G hata hapo ifikapo mwaka 2020.
Je Tanzania Tutapata Teknolojia Hii ya 5G ?
Ukweli ni ngumu kujua kwa asilimia 100 kama Tanzania tutakuwa na uwezo wa kutumia teknolojia ya 5G ifikapo mwaka 2020, ila kwa upande mwingine ni wazi kuwa mategemeo ya kupata teknolojia hii mapema ni madogo sana tena ukizingatia hadi sasa bado kampuni mbalimbali za kutoa huduma za simu zinatumia mtandao wa 3G pekee.
Pengine mategemeo makubwa ni kupata teknolojia ya 4.5G ambayo kwa jina lingine inaitwa 4G LTE – A ambayo hii nayo inakuja na kasi zaidi kuliko teknolojia ya 4G. Teknolojia ya 4.5G kwa sasa inatumiwa na nchi chache duniani ikiwa pamoja na korea ya kusini.
Je kuna Tofauti Gani Kati ya 4G na 5G ?
Kwa kuanza 5G ni teknolojia mpya hivyo ni teknolojia ambayo ni bei ghali sana kuiwezesha, tofauti na teknolojia ya 4G ambayo sasa imeenea zaidi duniani kote. Kingine kikubwa na kasi, 4G kasi yeke ni ndogo ukilinganisha na 5G inavyotegemewa kwani 4G inasemekana kuwa na kasi ya kudownload hadi MB 100 kwa sekunde huku kiwango cha chini cha 5G kinategemewa kuwa GB 1 hadi GB 10 kwa sekunde.
Tofauti na hayo zipo tofauti nyingi sana kati ya 4G na 5G lakini hizo hapo juu ndio tofauti kubwa na za muhimu kuhusu teknolojia ya 5G na 4G.
Kwa sasa hayo ndio baadhi tu ya mambo ambayo ya awali yanayoweza kukupa ufahamu kuhusu teknolojia ya 5G, Kwa sasa kama ulikuwa hujui kampuni nyingi za kutengeneza simu tayari zimesha anza kutengeneza simu zenye uwezo wa 5G moja kati ya kampuni ambazo zinategemewa kuwa na simu zenye 5G mapema ni pamoja na kampuni ya Nokia pamoja na Samsung.