Wakati kampuni ya Facebook ikiendelea na sakata la kuvujisha data za watumiaji wake zaidi ya milioni 50 kupitia kampuni ya Cambridge Analytica, huko nchini Misri mambo ni tofauti kidogo kwani wiki moja iliyopita serikali nchini humo imezindua mtandao wa kijamii maalumu kwaajili ya nchi hiyo.
Mtandao huo mpya unaofanana na Facebook umezinduliwa nchini Misri, kwa jina la EgFace. Hata hivyo mtandao huo wa kijamii unaonekana kutengenezwa mara baada ya Waziri wa mawasiliano nchini Misri kutangaza kuwa Misri itazindua mtandao wake wa kijamii.
Hata hivyo ripoti zinasema, Raia wa Misri walionyesha kukejeli na kutounga mkono uamuzi huo uliotangazwa tarehe 12 mwezi Machi, wengi wao wakiwa na mawazo kuwa, hatua hiyo ni ya makusudi kuwezesha vyombo vya usalama kufuatilia watumiaji wa mtandao huo , kukusanya taarifa na kufuatilia anuani za watumiaji.
Kwa sasa mtandao huo unapatikana kupitia anuani ya egface.com na tayari kuna watumiaji wa chache kutoka nchini humo wamesha anza kutumia mtandao huo, huku ikisemekana kuwa anuani nyingi za mtandao wa Facebook zimefungwa hivi karibuni na tayari watu wengine wamekamatwa kwa makosa ya ”uchochezi” dhidi ya serikali ya Misri,Jeshi na Polisi.