Kama wewe ni mmoja wa wabunifu wa programu, basi jina Github sio jina geni machoni kwako. Lakini kama wewe hujui kuhusu GitHub, huu ni mtandao ambao unasaidia wabunifu mbalimbali kushiriki ubunifu wao na watu mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza programu zao.
Mtandao huu umejaa wabunifu mbalimbali wadogo na wakubwa ikiwa pamoja na wabunifu kama Facebook, Uber, Google, Apache na wabunifu wengine mbalimbali ambao wanatengeneza programu ambazo ni chanzo wazi (Open Source).
Habari za hivi karibuni kutoka tovuti ya Bloomberg, zinasema kuwa inawezekana kampuni ya Microsoft imenunua mtandao wa GitHub na inawezekana kampuni hiyo kutangaza kuhusu kununua kampuni hiyo siku ya leo jumatatu. Bado haijajulikana Microsoft imenunua mtandao huo kwa kiasi gani, lakini inasemekana hapo awali mwaka 2015 kampuni hiyo ilikuwa na gharama ya dollar za marekani bilioni 2 sawa na shilingi za kitanzania Tsh Trilioni 460.
Hakuna taarifa kamili kama Microsoft imejiandaa kutangaza kuhusu ununuzi huo, huku taarifa hizi nazo zikiwa bado hazina uhakika kwa sababu ya kukosa maoni yoyote kutoka kwa wasemaji wa kampuni ya Microsoft pamoja na GitHub kama ilivyo tangazwa na tovuti ya Bloomberg.
Kama wewe ni mbunifu wa programu na ungependa kujua zaidi kuhusu hili endelea kutembelea Tanzania Tech tutakujulisha pindi tutakapo pata taarifa zaidi.