Kama ulikuwa ufahamu GePG kirefu chake ni Government e-Payment Gateway, huu ni mfumo wa malipo wa Serikali ambao kwa sasa ndio unaotumika kwa asilimia kubwa kufanya malipo kwenye sekta mbalimbali za malipo ya huduma za umma.
Kwa sasa Mfumo huu unatumika kwenye huduma mbalimbali za kilasiku kama vile huduma za kununua umeme wa luku, huduma za kulipia maji pamoja na huduma za kununua tiketi za Mabasi ya endayo kasi zinazotolewa na kampuni ya TTCL ambayo nayo pia inatumia mfumo huo wa malipo wa serikali maarufu kama GePG.
Karibia huduma zote hizo mwanzo zilikuwa zinatolewa na kampuni ya kutoa huduma za malipo ya kieletroniki ya hapa Tanzania ina yojulikana kama Maxmalipo. Sasa kwa mujibu wa tovuti ya Swahili Times, kampuni ya Maxmalipo hivi leo imewatangazia wafanyakazi wake kuwa inatarajia kupunguza wafanyakazi wake kutokana na kupungua kwa mapato kwenye kampuni hiyo.
Katika barua iliyotolewa kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo, imeeleza kuwa, inalazimika kufanya mabadiliko katika mfumo wake wa uongozi na utendaji kazi ili kuongeza ufanisi na kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Kutokana na mabadiliko hayo kampuni hiyo imelazimika kupunguza wafanyakazi ili isielemewe na mzigo wa kuwalipa kutokana na mapato kupungua. kampuni hiyo ambayo iliingia mkataba wa miaka miwili na Wakala wa Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi (UDART), katika kutoa huduma ya ukusanyaji wa nauli, iliacha kutoa huduma hiyo baada ya kumalizika kwa mkataba wake mapema mwaka huu.
Chanzo kingine cha kushuka kwa mapato ya kampuni hiyo kinadaiwa kuwa ni kuanzshwa kwa mfumo mpya wa malipo wa serikali, jambo lililosababisha mashirika na taasisi mbalimbali za serikali kucha kutumia huduma za kampuni hiyo na badala yake kuhamia katika mfumo mpya wa malipo wa serikali.