Kampuni ya Huawei hapo mwaka jana (2019) ilizindua mfumo wake wa uendeshaji wa HarmonyOS, mfumo huo ulizinduliwa mara baada ya kampuni hiyo kupigwa marufuku na Google tumia mfumo wa Android.
Hata hivyo baada ya Huawei kuzindua mfumo huo wa HarmonyOS, mara moja kampuni hiyo ilitangaza kuwa mfumo huo sio kwaajili ya simu bali ni kwaajili ya Smart TV zake ambazo zilitarajiwa kutoka baadae mwaka huo.
Lakini habari mpya hivi karibuni zinasema kuwa kampuni ya Huawei inategemea kuanza kutumia mfumo wake wa HarmonyOS kwenye simu zake kuanzia mwaka 2021. Kwa mujibu wa tovuti mbalimbali, mfumo huo wa HarmonyOS 2.0 unatarajiwa kufunguliwa (Open Source) kwa watumiaji mbalimbali kuanzia mwezi uliopita kwa ajili ya wabunifu wa programu kutengeneza programu mbalimbali juu ya mfumo huo.
Hata hivyo, mifumo ya Android na iOS imeweza kufanikiwa kwa sababu inayo mamilioni ya watengenezaji wanao tengeneza programu ambazo zinawekwa kwenye masoko ya Play Store na App Store. Kwa upande wa HarmonyOS, Huawei imesema kwa sasa inaweka jitihada katika kuleta mfumo huu kwenye vifaa vingi zaidi ili kuhakikisha inapata wabunifu wengi zaidi wa programu ambao watatumia mfumo huo ikiwa na soko lake la App Gallery.
Mbali na soko la App Gallery, Huawei inayo huduma zake nyingine kama vile huduma zke za ramani, pamoja na huduma nyingine za Huawei Mobile Services (HMS) ambazo ni sawa na huduma za Google Mobile Services ambazo uruhusu wabunifu wa programu kubuni programu zinazoweza kutumia ramani.
Hata hivyo habari zinasema HarmonyOS inategemewa kuanza kufanyiwa majaribio kwenye simu za Huawei Mate 40 na baadae simu za Huawei P30 na P40. Pia inasemekana baadhi ya simu zinazotumia mfumo wa EMUI 11 zitaweza kupata mfumo huo.