Kwa muda sasa nimekuwa nikipata maswali ya jinsi ya kupata mashine ya EFD, ingawa hatua hizi zinapatika kwenye tovuti mbalimbali lakini hebu kwa urahisi kabisa tujaribu kuziandika hapa.
Kwa kifupi kabisa EFD ni mashine zilizotengenezwa kwa ajili ya kutumika katika biashara kwa ajili ya kudhibiti mauzo na mfumo wa mali unaofuata masharti yaliyoelezwa na sheria. Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato mwaka 2012, mtoa huduma hapa Tanzania anapaswa kuwa na mashine ya risiti za kielekroniki (EFD) kuhalalisha mauzo anayofanya.
Mashine hizi huunganishwa na mfumo wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na kuwasilisha taarifa muhimu ambazo husaidia katika ukadiliaji wa kodi.
Mashine za Risiti za Kielektroniki (EFD) AWAMU YA PILI
Utekelezaji wa awamu ya pili ya Mashine za Risiti za Kielektroniki (EFD) ulianza tangu mwaka 2013 kwa lengo la kuongeza idadi ya wafanyabiashara ambao watatumia mfumo wa Mashine za Risiti za Kielektroniki kutoa risiti au ankara za kodi katika kila muamala unaofanyika. Awamu ya pili inajumuisha wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa na VAT unasimamiwa chini ya Sheria ya Kodi ya Mapato, kupitia Kanuni za Kodi ya Mapato (Mashine za Risiti za Kielektroniki), 2012.
Utekelezaji wa awamu ya pili ya Mashine za Risiti za Kielektroniki utajumuisha makundi yafuatayo;
i. Wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa katika kodi ya ongezeko la thamani wenye mauzo-ghafi ya Shilingi milioni 14 na zaidi kwa mwaka;
ii. Wafanyabiashara wanaofanya biashara katika maeneo maarufu ya Mkoa, waliobainishwa kwa kuzingatia kodi wanayolipa;
iii. Wafanyabiashara wanaoshughulikia sekta za biashara zilizochaguliwa kama vile Vipuli, Vifaa vya Ujenzi, Maduka Madogo, Vituo vya Petroli, Maduka ya Simu za Kiganjani, Maduka madogo ya jumla, Baa na Migahawa, Maduka ya Dawa, Maduka ya Vifaa vya Kielektroniki, nk.
Mfumo huu utaendelea na Mamlaka itakuwa inasajili taratibu wafanyabiashara kulingana na ustawi, uzoefu na uwezo wa biashara za wafanyabiashara hao
Kupata mashine za risiti za kielektroniki ni rahisi sana unahitaji kuwa na mambo machache sana ili uweze kuwezesha kupata mashine hiyo.
Kifupi Mahitaji ya EFD ni Haya
- Kiasi cha Fedha cha kununua Mashine hiyo (Angalia Wakala Hapa)
- Nakala ya namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN) (Unaweza Kupata Hapa)
- Namba ya usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
Kwa kampuni Unahitaji vyote hivyo hapo juu pamoja na
- Leseni ya Biashara (Unaweza Kupata Maelezo Hapa)
- Anwani sahihi ya mahali kampuni au taasisi inapo fanya biashara
Na hayo ndio maelezo mafupi jinsi ya kupata mashine hiyo ya EFD au Electronic Fiscal Devices, kama unataka maelezo zaidi unaweza kutembelea tovuti ya TRA au piga simu za bure kwa Tanzania 0800 750 075 au 0800 780 078.
Kwa habari zaidi za teknolojia hakikisha una download App ya Tanzania Tech kupitia Play Store pia usasahau kujiunga na channel yetu ya Tanzania Tech kupitia Youtube ili uweze kupata habari zote za teknolojia kwa njia ya Video.