Mkutano wa WWDC 2018 bado unaendelea huko San Jose Convention Center, California, nchini Marekani, ikiwa leo inakuwa siku ya pili ya mkutano huo ulio anza siku ya jana na ukitarajiwa kufikia ukomo wake siku ya tarehe 8 ya mwezi huu wa sita.
Kama ulifanikiwa kuangalia mkutano wa ufunguzi wa WWDC 2018 hapo jana, basi lazima utakuwa uliona baadhi ya mambo mapya ikiwepo ujio wa mfumo mpya wa uendeshaji wa iOS 12. Kwenye makala hii tutaenda kuangalia mambo yaliyo tangazwa yanayo tarajiwa kuwepo kwenye mfumo huo mpya wa uendeshaji wa iOS 12. Bila kupoteza muda twende tukangalie mambo hayo mapya.
Screen Time
Kwenye mfumo mpya wa iOS 12, Apple imejikita kuhakikisha unatumia kifaa kwa namna bora na kwa kuzingatia afya. Kipengele kipya cha Screen Time kwenye mfumo wa iOS 12 kitafafanua ni muda gani unatumia kwenye kifaa chako na pia itaonyesha ni muda gani unatumia kwenye programu mbalimbali. Sehemu hiyo pia inaweza kutenganisha matumizi ya programu kwa vikundi kama vile (michezo, mitandao ya kijamii nk) ikiwa pamoja na kufuatilia programu ambazo zinatuma taarifa (Notification) zaidi. Screen Time pia itatoa muhtasari wa kila wiki wa tabia zako za matumizi ya kifaa chako.
Kama ilivyo kwenye mfumo wa Android P, utaweza kuweka mipaka ya muda kwa kila programu unayo tumia. IOS itakupa taarifa moja kwa moja kama utakuwa umezindisha muda ulio jiwekea kwenye kila programu. Ujumbe wa “Muda Umeisha” utaonyeshwa kama muda ulio jiwekea utaisha na endapo unataka kuendelea kutumia programu hiyo, unaweza kuongeza muda kwenye programu husika.
Group Notification
Kwenye mfumo huu mpya wa iOS 12 Apple inakuja na njia mpya ya kuweza kudhibiti taarifa unazopata kwenye kifaa chako. Group Notification hii ni sehemu mpya ambayo itakusaidia kukusanya taarifa (notification) zote zinazo ingia kwenye kifaa chako kwa kuzipanga kwa vikundi (group) maalum. Kwa mfano kama unapata mchanganyiko wa taarifa (Notification) za whatsApp na meseji za kawaida kutoka kwa watu mbalimbali, sehemu hii ya Group Notification itakusanya taarifa zote za WhatsApp na kuziweka sehemu moja na taarifa zote za meseji za kawaida na kuziweka sehemu moja. Pia sehemu hiyo itakupa urahisi wa kufuta taarifa (Notification) nyingi kwa wakati mmoja.
Animoji Tongue Detection
Kupitia mfumo mpya wa iOS 12, Apple pia inaleta Animoji mpya za ghost, koala, tiger, pamoja na tyrannosaurus rex. Lakini kama haitoshi Apple imeongeza uwezo zaidi kwenye katuni za Animoji na sasa zitaweza kujua pale utakapo toa ulimi wako nje.
Memoji
Kwenye iOS 12, Apple imeleta aina mpya ya katuni za Memoji, kupitia sehemu hiyo utaweza kuunda Katuni za Memoji zinazofanana na wewe, Kupitia sehemu ya hiyo utaweza kuchagua rangi ya ngozi yako, macho, mdomo, nywele na vingine vingi ili kuweza kutengeneza sura ya katuni ya Memoji itakayo fanana na wewe.
Group Facetime
Kupitia programu ya Facetime, Apple imeleta maboresho zaidi kwenye programu hiyo kwa kuleta uwezo wa kupiga simu za Video kwa Kikundi. Kupitia programu hiyo utakuwa na uwezo wa kuunganisha hadi watu 32 kwa pamoja. Vilevile Apple imeleta muonekano mpya ambao utasaidia watu wote 32 kuweza kuonekana vizuri kwenye simu au kwenye kompyuta yako ya Mac pale unapokuwa unatumia sehemu hiyo ya Group FaceTime. Mbali na hayo utakuwa na uwezo wa kutumia katuni za Animoji au Memoji wakati unapiga simu za video kupitia programu ya Facetime.
Measure App
Kwenye maboresho mengine ya programu ni pamoja na ujio wa programu mpya ya Measure App, hii ni aina mpya ya programu itakayo kuwepo kwenye iOS 12 ambayo itakupa uwezo wa kufanya vipimo kwa kutumia kioo cha simu yako kwa kutumia teknolojia ya Ukweli ulioongezewa au kwa jina la kitaalamu AR au Augmented Reality.
Maboresho ya App ya Photos
Maboresho mengine ya programu ni pamoja na app ya Photos, ambayo sasa itakuwa na sehemu mpya ya “For You” ambayo itakuwa ikionyesha aina mbalimbali za Effect za kuweka kwenye picha zako, picha gani nzuri ya kushiriki kwenye mitandao ya kijamii, pamoja na mambo mengine mbalimbali yanayohusu picha ndani ya simu yako yenye mfumo mpya wa iOS 12.
Shortcut App
iOS 12 inakuja na maboresho pia ya Siri na baadhi ya maboresho hayo ni pamoja na ujio wa App mpya ya Shortcuts, App hii inakusaidia kuweza kutengeneza maneno binafsi ambayo utaweza kuyatumia pale unapotaka kutumia programu ya Siri.
Maboresho Mengine
Mboresho mengine ni madogo madogo ambayo ni pamoja na mabadiliko ya App ya Habari Apple News, Mbadiliko ya jina la programu ya iBooks na sasa itakuwa inaitwa Apple Books pamoja na Mabadiliko ya App ya Stocks, ikiwa pamoja na ujio wa App ya Voice Memo kwenye vifaa vya iPad. Mbali na hayo mabadiliko mengine ni pamoja na kuwepo kwa sehemu ya iCloud kwenye sehemu ya Voice memo ambayo utaweza kuhifadhi sauti zako kwenye iCloud.
Na hayo ndio mabadiliko makubwa ya mfumo mpya wa iOS 12 ambao unategemewa kuja rasmi mwaka huu kwa watumiaji wote wa vifaa vya iOS. Kupata habari zaidi za mkutano wa WWDC 2018 endelea kutembelea Tanzania Tech pia unaweza kutembelea ukurasa wetu maalum wa #WWDC 2018 ili kupata habari zaidi za mkutano huo.