Kampuni ya Facebook ambayo inamiliki mtandao wa WhatsApp, hivi karibuni ilikuwa na mpango wa kuweka matangazo kwenye programu yake ya WhatsApp. Lakini kwa mujibu wa tovuti ya The Wall Street Journal, inasemekana mpango huo kwa sasa umeahirishwa na programu ya WhatsApp itaendelea kutumika kama programu ya bure.
Kwa mujibu wa tovuti hiyo inawezekana kuwa, bado facebook inafikiria kuleta matangazo kwenye sehemu ya Status ndani ya programu hiyo, lakini hadi sasa bado hakuna muda maalum ambao umetangazwa wa sehemu hiyo mpya ya matangazo kuja kwenye programu hiyo.
Inasemekana kuwa wabunifu wa programu wa Facebook waliokuwa wanashulikia kutengeneza sehemu hiyo mpya ya matangazo wamepewa majukumu mengine, huku baadhi ya sehemu ambazo zilikuwa zimesha tengenezwa ndani ya programu hiyo zikiondolewa na kuacha programu hiyo ikiwa bila dalili yoyote ya kuwa na matangazo kwa siku za karibuni.
Kama unakumbuka, miaka miwili iliyopita mgunduzi mweza wa WhatsApp, Jan Koum alitangaza kuachana na kampuni ya Facebook huku moja ya sababu ikiwa ni baada ya kampuni ya facebook kuja na mpango wa kuonyesha matangazo kupitia programu hiyo. Hata hivyo inasemakana kuwa Koum alikuwa na wasiwasi wa usalama wa programu hiyo na kuamua kuachana na programu hiyo pamoja na kampuni ya Facebook kwa ujumla.
Kwa sasa inaonekana Facebook inatafuta njia nyingine za kutengeneza pesa kupitia programu hiyo, huku kwa sasa ikiwa imeangazia macho kwenye mfumo maalum wa kuunganisha biashara mbalimbali na mtandao huo, ikiwa na lengo la kurahisha mawasiliano kati ya mtumiaji wa WhatsApp pamoja na makampuni mbalimbali.
Mfano wa mfumo huo ni pamoja na mfumo wa kampuni ya Mawasiliano ya Afrika Kusini ya MTN ambao unaruhusu watumiaji kuweza kununua vocha za muda wa maongezi kupitia app ya WhatsApp.