Baada ya kuwa kwenye majaribio kwa muda mrefu hatimaye hivi leo kampuni ya Microsoft imetangaza ujio wa kivinjari kipya cha Microsoft Edge. Kivinjari hicho ambacho sasa kinakuja na muonekano mpya pamoja na logo mpya kime tengenezwa juu ya mfumo wa Google maarufu kama Chromium, mfumo ambao pia hutumika kutengeneza kivinjari cha Google Chrome.
Kama unavyoweza kuona hapo juu, logo ya kivinjari hicho sasa imebadilika kabisa kutoka logo ya zamani (upande wa kushoto) kuja kwenye logo mpya (upande wa kulia). Mbali na logo, mfumo mzima wa kivinjari cha Microsoft Edge umebadilika kabisa na utaweza kutumia mfumo huu kama unavyotumia kivinjari cha Chrome.
Utaweza kuinstall Extension kama vile IDM na Extension nyingine nyingi ambazo zinafanya kazi kwenye kivinjari cha chrome, mbali na hayo pia utaweza kuingia kwa kutumia akaunti yako ya Google na kuhamisha data za kivinjari chako cha Chrome kwenda kwenye kivinjari hicho kipya cha Microsoft Edge.
Kwa sasa tayari unaweza kupakua Kivinjari hiki kwenye kompyuta yako ya Windows na MacOS ambapo kwenye Windows kivinjari hiki kita kuwepo badala ya kivinjari cha zamani ambacho kipo kwenye kompyuta nyingi zenye mfumo wa Windows 10. Unaweza kupakua kivinjari hichi Hapa kama unatumia mfumo wa Windows na Hapa kama unatumia mfumo wa MacOS.
Kwa watumiaji wa Android unaweza pia kupakua kivinjari hichi kipya kupitia soko la Play Store kwa kutumia link hapo chini.
Kwa watumiaji wa Windows 7, Kivinjari hiki pia kinaonekana kufanya kazi kwenye mfumo huo japo kuwa mfumo huo ulisitishwa na Microsoft siku kadhaa zilizopita.