Makampuni ya mitandao ya simu nchini tanzania yametakiwa kulipa faini kutokana na kushindwa kutoa huduma zinazotakiwa na watanzania, ifuatayo ni barua ya (TCRA) Tanzania Communications Regulatory Authority kwa umma kuhusiana na taarifa hiyo. Barua hiyo ilitolewa tarehe 2.3.2016.
TAARIFA KWA UMMA
MAAMUZI YA KIDHIBITI YALIYOCHUKULIWA KWA WATOA HUDUMA WA SIMU KWA KUSHINDWA KUTIMIZA MASHARTI YA KANUNI ZA UBORA WA HUDUMA
- Kwa mujibu wa Majukumu na wajibu wa Mamlaka ya Mawasiliano katika kusimamia shughuli za Mawasiliano nchini, Mamlaka ilifanya zoezi la kutathmini ubora wa huduma za Mawasiliano (sauti na data) zinazotolewa na makampuni ya simu nchini kupata uhalisia wanaoupata watumiaji wa huduma hizo. Mamlaka ilitumia vipimo mahususi kutathmini ubora wa huduma zinazotolewa na makampuni ya simu kukidhi matakwa ya Kanuni za Ubora wa Huduma za Sheria ya Mawasiliano ya Kielectroniki na Posta za mwaka 2011. (Electronic and Postal Communications (Quality of Service) Regulations, 2011). Katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba, Mamlaka ilifanya ukaguzi wa vigezo vya Ubora wa huduma kwa maeneo ya jiji la Dar es Salaam. Makampuni yaliyoshirikishwa katika ukaguzi huu ni pamoja na Airtel (T) Ltd, Benson Informatics Ltd wajulikanao kama SMART, Millicom International Cellular (T) Ltd wajulikanao kama Tigo, Vodacom (T) Ltd na Zanzibar Telecom Ltd wajulikanao kama ZANTEL.
- Mnamo tarehe 18 Desemba, 2015 Mamlaka ilitoa Amri ya Utekelezaji (Compliance Order), kwa watoa huduma hao, kwa mujibu wa kifungu cha 45 cha Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA Act, 2003), Sura ya 172 kama ilivyobadilishwa na kifungu cha 179 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Electronic and Postal Communications Act, (EPOCA) Sura 306 ya Sheria ya Tanzania, ikiwataka watoa huduma kufika mbele ya Mamlaka tarehe 28mwezi Desemba, 2015 kujitetea kwa nini wasichukuliwe hatua za kisheria kwa kutotimiza/kushindwa kutimiza, kudharau kanuni za Ubora wa Huduma kwa kutozingatia vigezo vya ubora wa huduma vilivyowekwa na Mamlaka kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2015, kinyume na Kanuni ya 9 (jedwali la pili),10 (jedwali la tatu), na 11 (jedwali la nne) ya Kanuni za Ubora wa Huduma za Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta za mwaka 2011.
- Amri hiyo ya utekelezaji ilitolewa kwa Makampuni yote ya Simu husika na kukiri kupokelewa mnamo tarehe 21 Desemba, 2015 na Makampuni hayo kufika mbele ya Mamlaka kujitetea tarehe 28 Desemba, 2015 kama walivyoagizwa na wakakubali kushindwa kutimiza vigezo vya ubora wa huduma na kutoa utetezi kuwa hali hiyo ilisababishwa na sababu mbalimbali.
- Baada ya kuusikiliza utetezi wa Makampuni hayo ya simu na kutathmini pia utetezi wa maandishi uliowasilishwa Mamlaka kutoka kwenye makampuni husika, Mamlaka ilibaini pasipo na shaka kuwa, makampuni haya yalishindwa kutekeleza masharti na vigezo vya ubora wa huduma kwa mujibu wa Kanuni za Ubora wa Huduma za Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta za mwaka 2011. Kwa kuzingatia kukubali kutotimiza vigezo vya ubora wa huduma, na kusudio la Makampuni ya Simu husika kuahidi kuboresha vigezo vya ubora wa huduma; pamoja na kusikiliza utetezi wao na jitihada za kuboresha ubora wa huduma zao.
Mamlaka ya Mawasiliano imefanya uamuzi wa kutoa adhabu kwa mujibu wa kanuni za ubora wa huduma kama ilivyoainishwa katika Kanuni ya 15 ya Kanuni za Ubora wa Huduma.
- Vile vile, Kampuni za utoaji wa huduma za Mawasiliano ya simu zinawajibika kuhakikisha kuwa zinatoa huduma katika vigezo vilivyoainishwa katika kanuni za Ubora wa Huduma na ni wajibu kwa kila kampuni kufanya hivyo. Kushindwa kutimiza vigezo hivyo ni ukiukwaji wa masharti ya leseni pamoja na Kanuni za Ubora wa Huduma za Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta za mwaka 2011, Kanuni ya 9 (jedwali la pili) na Kanuni ya 10 (jedwali la tatu) na Kanuni ya 11 (jedwali la nne). Hii inaipa Mamlaka wajibu wa kutoza faini kwa mujibu wa kifungu cha 15 cha Kanuni za Ubora wa Huduma za Sheria ya Mawasiliano ya Kielektoniki na Posta.
- Kwa mujibu wa Kifungu cha 17 cha Jedwali la Pili la Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Sura ya 306 ambacho kinaipa nguvu za kisheria Mamlaka kutoa adhabu kwa kukiuka Masharti ya Leseni. Kwa hiyo Mamlaka:-
- A) Imetoa adhabu kwa:-
- Airtel Tanzania Limited,
- Benson Informatics Limited (Smart),
iii. MIC Tanzania Limited (Tigo),
- Vodacom Tanzanian Limited na
- Zanzibar Telecom Limited (Zantel).
Kwa kushindwa kutoa huduma kwa mujibu wa vigezo vya ubora wa huduma kwa mujibu wa Kanuni za Ubora wa Huduma za Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta za mwaka 2011. (Electronic and Postal Communications (Quality of service) Regulations, 2011).
- B) Aidha Mamlaka imezitaka Kampuni hizo:-
- Kuhakikisha huduma zao zinakidhi vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa Kanuni za Ubora wa Huduma katika kipindi cha miezi sita tangu siku ya tangazo hili.
- Kulipa faini zifuatazo katika kipindi cha mwezi mmoja tangu siku ya uamuzi huu:-
- Airtel Tanzania Limited – TZS. 22,500,000.00
- Benson Informatics Limited (Smart) – TZS. 12,500,000.00
- MIC Tanzania Limited (trading as Tigo) – TZS. 25,000,000.00
- Vodacom Tanzanian Limited – TZS. 27,500,000.00
- Zanzibar Telecom Limited (Zantel)– TZS. 25,000,000.00
- C) Kushindwa kwa Kampuni zilizotajwa hapo juu kulipa faini hizi, itapelekea Mamlaka kuendelea na utekelezaji wa sheria na maamuzi mengine kwao kwa mujibu wa sheria.
- Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inawakumbusha Watoa Huduma wote wa huduma za simu za mkononi kuhakikisha kuwa huduma zinatolewa kwa kuzingatia vigezo vilivyoainishwa kupitia Kanuni za Ubora wa Huduma. Mamlaka itaendelea kufanya uchunguzi wa ubora wa huduma sehemu mbalimbali nchini kila baada ya miezi mitatu. Endapo kampuni za kutoa huduma za simu zitaendelea kutoa huduma bila kufikia vigezo vilivyoainishwa, Mamlaka ya Mawasiliano itachukua hatua zaidi za kisheria ikiwemo kufuta leseni zao.
IMETOLEWA NA;
Dkt. Ally Y. Simba
MKURUGEZI MKUU
02/03/2016