Kampuni ya Samsung bado inaendelea kuzindua simu zake mpya za bei nafuu, siku za karibuni kampuni hiyo ilizindua simu mpya ya Galaxy M31 simu ambayo ni toleo la maboresho la simu ya Galaxy M30 iliyo zinduliwa mwaka jana 2019.
Lakini kama haitoshi hivi karibuni kampuni ya Samsung inatarajia kuja na toleo jipya la simu ya Galaxy M21, simu ambayo itakuwa ni toleo la maboresho la Galaxy M20 iliyotoka mwaka jana 2019. Kwa mujibu wa tovuti ya GSMArena, Galaxy M21 inatarajiwa kuja na maboresho kadhaa ikiwa pamoja na kioo na battery kubwa, pamoja na kamera tatu kwa nyuma.
Kwa mujibu wa tovuti hiyo, Galaxy M21 ambayo inategemea kuzinduliwa huko nchini India, itakuja na kamera tatu kwa nyuma huku kamera kuu ikiwa na Megapixel 48 na nyingine mbili zikiwa na uwezo wa Megapixel 8 na Megapixel 5. Kamera zote zinakuja na uwezo wa kuchukua video za hadi 4K au 2160p@30fps.
Upande wa sifa za ndani, Galaxy M21 inategemea kuja na processor ya Exynos 9611 ambayo inasaidiwa na RAM ya GB 4 huku ikiwa na toleo lingine lenye RAM ya GB 6. Kwa upande wa uhifadhi wa ndani simu hii inatarajiwa kuja na uhifadhi wa hadi GB 128 huku ikiwa na toleo lingine lenye GB 64
Simu hii inatarajiwa kuja na battery kubwa ya mAh 6000, yenye uwezo wa fast charging hadi W15. Simu hii pia itakuja ikiwa na Radio FM, ikiwa pamoja na tundu la kuchomeka headphone maarufu kama headphone jack. Galaxy M21 inategemea kwanza kupatikana kwanza kwa nchini India na baadae kusamba kwenye nchi mbalimbali ikiwepo Tanzania.
Kujua zaidi kuhusu sifa kamili pamoja na bei ya simu hii hakikisha unaendelea kutembelea Tanzania Tech kwani tutakujuza pindi tu simu hii itakapo zinduliwa rasmi hapo Tarehe 16 Machi 2020.