Baada ya kampuni ya Google kuzindua mfumo wa Android 9 (Pie) hapo mwaka jana (2018), Hatimaye Google imeanza kufanyia kazi mfumo mpya wa Android ambao unasemekana kupewa jina la Android Q.
Kwa kawaida Google hutoa mfumo mpya wa Android kila mwaka na kama mambo yatakuwa kama yanavyo tarajiwa pengine mwishoni mwa mwezi wa tano tunaweza kupata kujaribu mfumo huo kwenye baadhi ya simu. Lakini kabla ya kusubiria hadi mwezi huo yafuatayo ni machache ambayo yamegundulika kuja kwenye mfumo huo mpya wa Android Q.
TABLE OF CONTENTS
Dark Mode
Dark mode ni moja kati ya sehemu mpya inayo tegemewa kuwepo kwenye mfumo mpya wa Android Q, Sehemu hii urahisha mtu kuweza kutumia simu vizuri hasa wakati wa usiku kwani sehemu hii huwezesha mwanga mweusi kwaajili ya kulinda macho yako hasa unapokuwa una angalia simu yako kwa muda mrefu.
Sehemu hii pia mbali ya kuwepo kwa ajili ya kulinda Afya ya macho yako, sehemu hii pia inaweza kusaidia sana simu kudumu na chaji kwa muda mrefu pale unapokuwa umewasha sehemu hiyo. Kwa wale ambao watafanikiwa kuwa na simu mpya ya Galaxy S10, sehemu hii inategemewa kuwepo ndani ya mfumo mpya wa Samsung One UI, lakini hautakuwa unafanya kazi kwenye simu nzima kama inavyo tegemewa kwenye mfumo mpya wa Android Q.
Kwa mujibu wa tovuti ya Xda Developers, Kama unavyoweza kuona kwenye picha hapo mfumo wa Android Q unategemea kuweka sehemu ya Dark Mode kila sehemu hadi kwenye sehemu ya mpangilio au Settings. Mbali na sehemu hiyo ya Settings, pia inasemekana sehemu hiyo itaweza kuweka mwanga mweusi hadi kwenye baadhi ya Apps ambazo hazina uwezo wa kuweka mwanga huo kwa ajili ya kulinda afya ya macho.
Kama unataka kujua jinsi sehemu hii inavyofanya kazi unaweza kubofya alama ya mwezi iliyoko upande wa kulia wa tovuti hii ya Tanzania Tech, au kama unatumia app ya Android ya Tanzania Tech bofya sehemu ya Mpangilio > Kisha bofya Soma Usiku.
Aina Mpya ya Ruhusa
Kama tunavyojua siku hizi ukipakua app baada ya ku-install wakati unawasha app hiyo utaulizwa ruhusa (Permissions) mbalimbali ambazo hizi husaidia apps hizo kufanya kazi kwa usahihi. Lakini pia ziko baadhi ya apps ambazo hutaka ruhusu hizi na kuzitumia vibaya kama inavyosemekana kwenye app ya Facebook.
Sasa kuliona hilo, inasemekana Google inakuja na mabadiliko mapya kwenye mfumo wa Android Q ambapo kutakuwa na aina mpya ya ruhusa ya ( allow only while the app is in use ) ambayo hii itaruhusu apps kutumia ruhusa yoyote pale unapokuwa unatumia app hiyo tu, na pale unapo maliza kutumia app husika basi ruhusa hiyo huzimwa kwenye app hiyo.
Ruhusa hii itasaidia sana kwa apps zile ambazo hutumika kufanya udukuaji kwenye simu yako kwani apps hizo zitashindwa kuwa na ruhusu za muhimu za kuingia kwenye baadhi ya sehemu za muhimu za simu yako.
Sehemu Nyingine Mbalimbali
Sehemu nyingine zinazo tarajiwa kufanyiwa maboresho kwenye mfumo wa Android Q, ni pamoja na ujio wa sehemu mpya ya kutumia simu kwenye kompyuta, sehemu ambayo itakuwa inafanya kazi kama Samsung DeX inayopatikana kwenye simu za Galaxy Note 8, Galaxy Note 9 na Galaxy S9 na Galaxy S10 inayotarajiwa siku chache zijazo.
Mbali na hayo, sehemu nyingine inayo tegemewa ni sehemu ya mpya ya kurekodi screen ambayo itakuwa inapatikana moja kwa moja kwenye mfumo wa Android Q. Kwa sasa wengi mnajua kuwa ili kurekodi screen ya simu yako inakupasa kuwa na app kama AZ Screen Recorder ambayo hii ukupa urahisi wa kurekodi kioo cha simu yako kwa haraka.
Kama unavyoweza kuona hapo juu kwa sasa sehemu ya kurekodi itakuwa ndani ya mfumo wa Android Q hivyo utakuwa huitaji ku-install app yoyote.
Haya yote ni baadhi tu ya mambo yanayotegemewa kwenye mfumo mpya wa Android Q, ili kupata picha kamili ya Android Q itabidi kusubiri kidogo hadi pale itakapo fikia kwenye hatua za majaribio ya mfumo huu. Kwa sasa hayo ndio machache ambayo tumefanikiwa kuyajua hivyo endelea kuwa nasi tutakupa habari zaidi za mfumo huu mpya pindi tu tutakapo zipata.