Kwa sasa karibia kila programu ya muhimu kwenye simu yako inakuja na muonekano wa giza au dark mode, hivi karibuni Google imatangaza kuwa mfumo mpya wa Android 10 utakuja na sehemu ya kuwasha muonekano wa giza, kama haitoshi mfumo mpya wa iOS 13 pia unakuja na muonekano wa giza.
Kama unavyoweza kuona ni wazi kuwa muonekano wa giza ni muhimu kwa watumiaji mbalimbali wa programu pengine ndio maana Instagram nayo inajiandaa kuja na muonekano huo wa giza kwenye programu zake.
Kwa mujibu wa tovuti ya Android Police, Instagram kwa sasa inafanya majaribio ya muonekano huo wa Giza ambao tayari unapatikana kwa baadhi ya watumiaji wa simu zenye mfumo wa Android 9 (Pie) pamoja na baadhi ya watumiaji wa mfumo wa iOS 13. Unaweza kuona picha ya muonekano huo kupitia hapo chini.
Kwa sasa inasemekana muonekano huo utakuwa unafanya kazi sambamba na sehemu ya kuwasha muonekano wa giza inayopatikana kwenye mifumo wa Android na iOS. Hii ina maana kuwa instagram haitakuwa na sehemu ya kuwasha na kuzima muonekano huo bali mtumiaji anatakiwa kuwasha muonekano huo kupitia simu yake kama inayo sehemu hiyo.
Kwa sasa mfumo wa Android 9 (Pie), Android 10 na mfumo wa iOS 13 yote inakuja na sehemu ya kuzima na kuwasha Dark Mode hivyo kama kifaa chako kina sehemu ya Dark Mode basi ni wasi kuwa muonekano huo mpya wa Instagram utafanya kazi kwenye kifaa hicho.
Bado hakuna tarehe halisi ya lini sehemu hii itawafikia watumiaji wote wa App za Instagram kujua zaidi kuhusu hilo hakikisha unaendelea kutembelea tovuti ya Tanzania Tech kila siku.