Huduma za usafirishaji kwa njia ya kidital zinazidi kuja hapa Tanzania, siku za karibuni kumeonekana kuwepo kwa ongezeko kubwa la kampuni nyingi ambazo zimejikita kutoa huduma za usafirishaji wa abiria hasa kwa kutumia app mbalimbali.
Sasa hivi karibuni, huduma hizo zinatarajiwa kuongezeka zaidi kwani kampuni mpya ya usafirishaji wa abiria yenye makao yake makuu nchini Kenya Little Ride, inategemea kuanza kutoa huduma zake jijini dar es salaam hivi karibuni.
Kwa mujibu wa tovuti ya The Citizen, Tofauti na kampuni nyingine kampuni hiyo ya Little inategemewa kutoa huduma bora huku ikisemekana kuwasaidia zaidi madereva kupata kipato kwa kuja na huduma za zaidi kama vile huduma ya kuuza muda wa maongezi, pamoja na kuuza bima mbalimbali kwa ajili ya wateja, pia inasemekana madereva wataweza kuwa mawakala ambao wanaweza kutumiwa na wateja kuweza kulipa bili mbalimbali.
Mtendaji mkuu wa kampuni hiyo ya Little, Kamal Budhabhatti alisema “Madereva wetu ni mawakala, wao wanaweza kuuza bima kwako, wanaweza kuuza airtime, wanaweza kulipa bili ya umeme na maji kwa ajili yenu na wanaweza kufanya mambo yote madogo, na hivyo huongeza mapato yao,”alisema mtendaji huyo.
Huduma za usafiri kwa njia ya kidigital zimeonekana kuwa na ushindani mkubwa sana hapa Tanzania, kwani siku za karibuni kampuni ya Uber imetangaza kuja na promosheni ya kutoa usafiri wa Uber Poa bure kuanzia saa tisa mchana, huku kampuni ya Taxify nayo ikitangaza kubadilisha jina na kuitwa Bolt kwa ajili ya kuboresha zaidi huduma zake.
Mbali na Tanzania, kampuni ya Little pia inategemea kuanza kutoa huduma zake nchini Ghana ifikapo mwezi May mwaka huu 2019.