Kampuni ya Huawei hivi karibuni kupitia kwa viongozi wake wa juu imebainisha kuwa inafikiria kutafuta mteja wa kununua biashara yake ya 5G. Huawei ni moja kati ya kampuni chache ambazo zina tengeneza teknolojia pamoja na vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha mtandao wa 5G.
Kwa mujibu wa tovuti ya mobileworldlive, kupitia mahojiano na mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo Ren Zhengfei, Huawei inafikiria kuiuza biashara yake hiyo huku ikifikiria zaidi kupata mteja kutoka nje ya bara la Asia. Hata hivyo inasemekana kuwa kampuni hiyo imedhamiria zaidi kuuza biashara yake kwa kampuni yoyote inayotokea “Magharibi”.
Kwa sasa inasemekana bado hakuna mnunuaji yoyote aliyelengwa kununua biashara hiyo, ingawa kampuni ya Huawei inasema kuwa inatarajia kutoa vibali vyote ikiwa pamoja na kutoa ruhusa kwa mnunuaji atakaye nunua biashara hiyo kubadilisha kitu chochote kwenye mtandao huo.
Hadi sasa bado kampuni ya Huawei haijatangaza kiasi gani cha pesa kinachohitajika kununua biashara hiyo ya 5G, hiI ikiwa inaonyesha kuwa kampuni hiyo bado iko kwenye mawazo ya kuuza biashara hiyo na pengine ikasitisha kabisa zoezi hilo.
Huawei imekuwa kwenye vita vya kibiashara na serikali ya marekani, vita ambavyo vinaonekana kuadhiri biashara mbalimbali za kampuni hiyo ikiwa pamoja na kuweka vikwazo kwenye biashara hii ya mtandao wa 5G na kuzuia kuendelea kwa baadhi ya nchi ambazo zinaiunga mkono serikali ya marekani.
Hivi karibuni kampuni ya Huawei ilitangaza kuwa, Simu yake mpya ya Huawei Mate 30 itakuja bila huduma za Google ikiwa pamoja na Play Store, Gmail, YouTube, Chrome pamoja na huduma nyingine nyingi ambazo zinakuja kwenye simu nyingi za Android. Mbali na hayo inasemekana kuwa simu hiyo itakuja na mfumo mpya wa Android na pia huwenda simu hiyo ikawa moja kati ya simu ambazo zitapata mfumo mpya wa Android 10.
Kupata habari zaidi kuhusu kuuzwa kwa biashara hiyo pamoja na habari kuhusu simu hiyo mpya ya Huawei Mate 30, hakikisha unaendelea kutembelea Tanzania Tech kila siku tuakujuza habari zote hizo pamoja na nyingine nyingi.