Hivi karibuni kampuni ya Huawei iliripotiwa kuwa kwenya hatua za mwisho za kukamilisha mfumo wake mpya wa uendeshaji ambao unaitwa Hongmeng OS. Mfumo ambao ndio ulikuwa mbadala wa mfumo wa Android ambao kwa kipindi hicho ulikuwa umesitishwa na Google baada ya katazo la raisi wa marekani.
Sasa habari mpya kutoka tovuti ya The Verge zinadai kuwa, msemaji wa kampuni hiyo amebainisha kuwa mfumo huo ambao bado uko kwenye hatua za matengenezo sio maalum kwaajili ya simu, wala mfumo huo haujatengenezwa maalum kwaajili ya kuwa mbadala wa mfumo wa Android.
Kwa mujibu wa makamu wa raisi wa kampuni ya Huawei Catherine Chen, kampuni hiyo haijapanga kutumia mfumo huo kama mbadala wa Android na kampuni hiyo itaendelea kutumia mfumo wa Android kama mfumo wa simu zake mpya. Hata hivyo kwa mujibu wa mwenyekiti wa Huawei, mfumo huo wa Hongmeng OS umetengenezwa maalum kwaajili ya matumizi ya ndani ya kampuni na hivyo bado kampuni hiyo haija amua kama mfumo huo utatumika kwenye simu zake.
Hatua hii imekuja wiki chache baada ya raisi wa marekani Donald Trump kutoa tamko kupitia mkutano wa G20, tamko ambalo linaruhusu kampuni ya Huawei kuendelea kufanya biashara na kampuni za marekani mara baada ya kuzuiwa wiki kadhaa kufanya biashara na kampuni za marekani.
Hata hivyo kwa mujibu wa wataalamu wa mambo ya teknolojia, inasemekana kuwa Huawei imechukua hatua za kusema hivyo ili kuficha siri zake za kibiashara kwani ni wazi kampuni hiyo ingepitia vikwazo vingi kwani mfumo huo usinge kubalika kwenye nchi mbalimbali tena hasa kipindi hichi ambapo kampuni hiyo bado iko kwenye migogoro na serikali ya marekani.
Kwa sasa hakuna anaejua sababu halisi kwanini Huawei imeamua kubadilisha kauli yake, wakati siku za karibuni mmoja wa wasemaji wake alinukuliwa na Reuters akisema mfumo huo utakuwa tayari kutumika kwenye simu zake ndani ya muda mfupi baada kampuni hiyo kuzuiwa kutumia mfumo wa Android. Kwa sasa hadi tutakapo jua zaidi, hayo ndio machache kuhusu mfumo wa Hongmeng OS.
Nimependeza na hii asante