Habari ya jumapili mwana teknolojia, leo tunaungana tena kwenye makala nyingine inayohusu pesa mtandaoni. Siku ya leo nimekuandalia hatua za kufuata ili kuweza kupata pesa mtandaoni kwa urahisi. Hatua hizi ni za muhimu sana na zinaweza kukusaidia sana kama wewe umeamua kujikita kwenye maswala mazima ya kufanya biashara mtandaoni.
Kumbuka ni vizuri kusoma hatua zote hizi ili kuweza kujua namna ya kuanza ikiwa pamoja na jinsi ya kuendelea kufanya biashara hiyo na kupatasa pesa kupitia mtandao, basi bila kupoteza muda twende tukangalie mambo haya muhimu.
1. Weka Malengo na Nia
Malengo na nia ni jambo la msingi kwenye biashara yoyote, hakikisha kama unataka kufanya biashara mtandaoni unajiwekea nia na malengo ili iweze kukusaidia baadae. Ukweli ni kwamba itafika wakati utakata tamaa kabisa lakini malengo na nia vitakurudisha kwenye mstari na utajikuta unaendelea, pia ni muhimu sana kuhakikisha angalau unapenda hicho unachokifanya kwani kwa mara ya kwanza hutoweza kupata pesa kwa haraka bali inakubidi kuendelea kukifanya kwa mapenzi na pesa itakuja baadae. Hii pia itakusaidia kurudi kwenye mstari pale utakapo kata tamaa.
2. Nunua Kompyuta
Kama unataka kufanya biashara mtandaoni na kupata pesa mtandaoni ambayo inaweza ikaendelezea maisha yako ya kila siku basi ni muhimu sana kuondoa mawazo kwamba utaweza kutengeneza pesa mtandaoni kwa kutumia simu yako ya mkononi.
Hakikisha unapata kompyuta kwani kompyuta ndio inayoweza kukusaidia sana kwenye mambo ambayo pengine usingeweza kuyafanya ukiwa kwenye simu yako ya mkononi. Simu yako ni ya muhimu pia lakini yenyewe inatumika kufanya kazi za ziada na sio kufanya kazi yote kwa asilimia 100.
Kuna aina nyingi za kompyuta hivyo usiingie gharama kununua kompyuta ya bei ghali unaweza kupata kompyuta ya kawaida yenye uwezo wa kufanya mambo ya kawaida kama kutembelea tovuti, kuandika barua pepe, kuangalia video pamoja na mambo mengine mbalimbali kulingana na kazi unayotaka kufanya mtandaoni.
3. Kuwa na Kiwango Fulani cha Pesa ya Kuanzia
Naposema pesa mtandaoni nadhani unanielewa, kama hujanielewa labda nikufafanulie kidogo. Kupata pesa mtandaoni kuna husisha mtandao au (Internet) na ili uweze kujiunga na Internet kwaajili ya kuendeleza biashara yako unahitaji pesa. Hivyo basi ni wazi kuwa unahitaji pesa ya kuanzia na sina maana unahitaji mamilioni au malaki hapana, unahitaji angalau Tsh 2000 hadi Tsh 5000 kwa wiki.
Hii inaweza kusaidia kujiunga na bando ndogo ndogo kwaajili ya kuangalia hali ya biashara yako au kwaajili ya kufanya kile unachotaka kulingana na aina ya biashara unayofanya mtandaoni.
Kumbuka kiwango cha pesa kina tofautiana kwa kila biashara hivyo ni vyema ukajua aina ya biashara yako mapema ili kuweza kujua ni kiwango gani cha pesa unahitajika kuwa nacho ili kuanza biashara yako ya mtandaoni na kupata pesa. Kwa mfano kama biashara yako ni YouTube basi ni wazi itakuhitaji kuwa na pesa nyingi zaidi kwani bando linalo hitajika kupakia video kwenye mtandao huo ni kubwa ukilinganisha na shughuli zingine.
4. Usifanye Biashara ya Mtandaoni Peke Yake
Napenda nikushauri na ningependa uwe makini sana kwenye hili, Hata mara moja usijikite kwenye biashara ya mtandaoni kwa asilimia 100. Kama wewe una familia au unategemewa kufanya mambo mbalimbali basi hakikisha unakuwa na mambo mengine ya kukuingizia pesa tofauti na kupata pesa mtandaoni. Kwenye hili ndipo malengo na nia vinapo kutana, kama una nia ya kitu na unamalengo nacho na unakipenda basi hata kama unaenda kazini utaweza kutenga muda wa kufanya kitu hicho hata kama kwa dakika tano.
Hii ni muhimu kwani biashara za mtandaoni hazitumi muda mfupi na kuanza kukuingizia pesa hapana, biashara hizi hutumia muda mrefu na inategemeana na aina ya biashara wakati mwingine biashara nyingine zinaweza kuchukua hadi miaka mitano.
Kwa mfano channel ya mtangazaji millard ayo ilitengenezwa mwaka 2012, hadi kufikia mwaka 2015 ndipo ilianza kufuatiliwa na watu wengi na pia ndipo ilipo anza kuonyesha mafanikio zaidi. Kama wewe ni mmoja wa watu ambao bado ni tegemezi (wanoishi nyumbani) au unasoma unaweza kutumia nafasi hiyo kuanza biashara yako ya mtandaoni sasa kwani inaweza kusaidia sana baadae.
5. Hakikisha Biashara yako Inatatua Changamoto za Watu Walio Kuzunguka
Hili ndio la mwisho kwenye list hii lakini pia hili ndio la muhimu zaidi, Kwenye kila biashara unayo ifanya iwe ya mtandaoni au biashara ya kawaida, Ili kufanikiwa mtandaoni hakikisha biashara unayotaka kuanzisha inaweza kutatua changamoto za watu walio kuzunguka. Biashara kama haitatui matatizo ya mahali ilipo basi ni ngumu sana kwa biashara hiyo kufanikiwa.
Kwa mfano kama unataka kuanzisha channel ya YouTube ni vyema kuhakikisha channel hiyo imejikita kusaidia watu kwenye mambo mbalimbali, kama unataka wafuatiliaji wa kudumu ni vyema uwe na kitu kitakacho wafanya waendelee kufuatilia channel yako kila siku. Vilevile watu hupenda kulinganisha mambo hivyo uzito wa msaada wako ndio utakao kufanya uweze kufanikiwa kwa haraka zaidi.
Pia hakikisha kwa mara ya kwanza usiweke sana pesa mbele kwa wakati ukiwa mchanga kwenye biashara yoyote ni watu wa chache sana wanaweza kuona thamani yako hivyo hakikisha angalau kwa mara ya kwanza unatoa huduma zako bure ili kuweza kuvutia kwanza wateja wako na kuwapa sababu kwanini walipie ili kupata huduma yako.
BONUS
Kama unataka kufanya biashara yoyote iwe ya mtandaoni au ya kawaida ni vyema kumtafuta mtu au biashara kama yako ya kuifuatilia. Ni kweli kwamba hakuna biashara mpya biashara zinafanana utofuti uliopo ni kuwa inawezekana mwenzako anafanya biashara kwa namna ya tofauti lakini msingi wa biashara unafanana.
Ni vyema kutafuta biashara ya mtandaoni ambayo inalingana na ya kwako kisha ifuatilie na utaweza kujifunza mambo mbalimbali ambayo yatakusaidia kwenye biashara yako ya mtandaoni unayo tarajia kuanza.
Natumaini mambo haya yanaweza kukusaidia kuanzisha biashara yako ya mtandaoni kwaajili ya kupata pesa mtandaoni. Kama unataka kupata mawazo ya aina za biashara za kufanya mtandaoni ili kupata pesa unaweza kusoma makala hii hapa.
Kama unayo maoni maswali au hata ushauri, tutafurahi sana ukituandikia kupitia sehemu ya maoni hapo chini au kupitia mitandao yetu ya kijamii. Kwa sasa pia Tanzania Tech inapatikana kupitia Telegram hivyo kama una maswali au chochote unachotaka kutujulisha unaweza kujiunga nasi kupitia link hii t.me/tanzaniatech. Basi mpaka siku nyingine endelea kutembelea Tanzania Tech.
Nice
Napenda Sana kufuatilia mtandao huu wa Tanzania tech swali langu linahusu) Btc Bitcoin inafanyikaje huwa naona tu matangazo
Sielewi his appy