Kivinjari cha Google Chrome ni moja kati ya programu za aina hii zinazo tumiwa na watu wengi zaidi kwa sasa, Miaka 10 iliyopita kisakuzi hicho kilizinduliwa rasmi na sasa kimekuwa ni kisakuzi maarufu zaidi duniani kwa kuwa na watumiaji zaidi ya Bilioni 1.
Leo tarehe 5 ya mwezi wa tisa kisakuzi hicho kimetimiza umri wa miaka 10 toka kuanzishwa kwake na katika kusherekea hayo kampuni ya Google imetangaza kuja na mabadiliko kadhaa kwenye kisakuzi hicho ikiwa pamoja na muonekano mpya kabisa na rahisi kutumia.
Mabadiliko hayo ni pamoja na mabadiliko ya muundo wa kivinjari hicho, ambapo baadhi ya icon zimebadilishwa, sehemu za tabs zimekuwa na muonekano wa tofauti na kwa watumiaji wa kisakuzi cha Google Chrome kwenye mfumo wa iOS wataona mabadiliko ya sehemu ya toolbar sasa itakuwa kwa chini tofauti na sasa ambapo sehemu hiyo iko kwa juu.
Mabadiliko mengine ni sehemu ya Password Manager, ambayo sasa imeboreshwa zaidi kwa kuekewa uwezo wa kukusaidia kutengeneza password ambayo itakuwa ni ngumu mtu kuweza kudukua. Vilevile sehemu hiyo ya Password Manager itasaidia kuhifadhi password zako na kuruhusu kuweza kuzitumia kila mara unapo hitaji.
Mabadiliko mengine yatahusisha sehemu ya Omnibox, kama ulikuwa ufahamu sehemu hii ni ile ambayo inatoa matokeo ya kitu unachotafuta kabla ya kubofya sehemu ya go. Sehemu hii kwa sasa imeboresho zaidi na itakuwa na uwezo wa kuonyesha matokeo ya vitu au watu kwa haraka zaidi.
Hayo ni baadhi ya mabadiliko machache ambayo yamefanyika kwenye kivinjari hicho cha Google Chrome. Mabadiliko haya na mengine mengi yatakuwepo kwenye toleo la Chrome 69 ambalo litapatikana kwa watumiaji wa vifaa vyote vya Android, iOS, Windows, Linux pamoja na MacOS.
Kwa sasa toleo hilo bado halijawafikia watu wote hivyo endelea kusubiri hivi karibuni utaweza kupata mabadiliko hayo kwenye kifaa chako chochote kinachotumia kivinjari cha Google Chrome.