Programu maarufu ya GBWhatsApp ambayo imejizolea umaarufu mkubwa miongoni mwa watumiaji mbalimbali wa simu za Android, hivi karibuni imetangazwa kusitishwa moja kwa moja. Kama wewe ni mtumiaji wa programu hiyo inawezekana kwa namna moja ama nyingine hujaona mabadiliko yoyote kuhusu programu hiyo lakini habari ikufikie kuwa programu hiyo haito endelea kuboreshwa na pengine hivi karibuni itaacha kufanya kazi kabisa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ukurasa wa telegram wa mbunifu wa programu hiyo, GBWhatsApp imesitishwa kuanzia siku ya jana tarehe 1 mwezi nane, ikiwa pamoja na akaunti zote za mitandao ya kijamii iliyokuwa inahusiana na programu hiyo.
Hadi sasa bado hakuna taarifa rasmi za kwanini mbunifu wa programu hiyo ameamua kuachana na uboreshaji wa programu hiyo, huku baadhi ya tetesi zikisema ni kutokana na Facebook kumshitaki mbunifu huyo mara baada ya kuendelea kuhamasisha utumiaji wa programu hiyo hata baada ya Facebook kutangaza kufungia watumiaji wa programu hiyo kutumia programu ya kawaida ya WhatsApp.
Kwa sasa inawezekana kabisa programu hiyo inaendelea kufanya kazi kama kawaida, lakini inawezekana siku za karibuni programu hiyo ikashindwa kuendelea kufanya kazi kwa asilimia 100.
GBWhatsApp ni programu iliyokuwa imetengenezwa juu ya programu ya kawaida ya WhatsApp huku ikikupa sifa za nyongeza kama vile kupakua Status, kuzima last seen pamoja na mambo mengine mengi ambayo hayapo kwenye programu ya kawaida ya WhatsApp.
Hata hivyo programu nyingine kama hii ya WhatsApp Plus yenyewe bado inaendelea kufanya kazi ila nadhani siku sio nyingi programu hiyo nayo itazimwa. Kama wewe ni mtumiaji wa programu hizi nadhani ni wakati sasa wa kurudi kutumia programu za kawaida za WhatsApp na WhatsApp Business. Kujua zaidi kuhusu hili endelea kutembelea tovuti ya Tanzania Tech kila siku.