Habari mpya kutoka mitandaoni zinasema kuwa kampuni ya Facebook inajiandaa kuja na pesa yake ya kimtandao maarufu kama (Cryptocurrency), ambayo itakuwa inatumika kwenye malipo ya bidhaa mbalimbali mtandao pamoja na kwenye mitandao yote inayomilikiwa na Facebook.
Kwa mujibu wa tovuti ya Wall Street Journal, inasemekana kuwa Facebook kwa sasa imeshanza kuajiri makampuni ya kifedha pamoja na makampuni ya biashara mtandaoni ili kuwezesha na kusaidia kutengeneza pesa hiyo mpya ya kimtandao.
Kwa sasa zoezi zima la utengenezaji wa pesa hiyo limepewa jina la Project Libra, ambapo zoezi hilo likikamilika litawapa fursa watumiaji wa mtandao kuweza kutumiana pesa hiyo baina yao, ikiwa pamoja na kununua bidhaa mbalimbali kupitia tovuti mbalimbali.
Facebook tayari imesha anza kufanya mazungumzo na tovuti na apps za biashara mbalimbali mtandaoni ili kuhakikisha zinawezesha aina hiyo ya malipo kutoka Facebook pale itakapo kamilika.
Kwa mujibu wa tovuti hiyo ya WSJ (Wall Street Journal), inasemekana kuwa Facebook pia inafanya mazungumzo na taasisi kubwa za kifedha kama Visa Inc na Mastercard Inc ili kuhakikisha thamani ya pesa hiyo ya kimtandao inabaki kuwa imara tofauti na Bitcoin ambayo thamani yake inapanda na kushuka kwa kasi kila siku.
Pia inasemekana kuwa Pesa hiyo ya kimtandao itakuwa inatumika kwenye mitandao yote inayo milikiwa na Facebook kama njia ya malipo ya matangazo, ikiwa pamoja na njia ya kuongeza watumiaji wa mitandao hiyo kwa kuwapa token kama zawadi kila wanapo fanya mambo mbalimbali kwenye mitandao hiyo kama vile kuangalia matangazo na kununua bidhaa iliyopo kwenye tangazo husika.
Kwa mujibu wa WSJ, hakuna msemaji yoyote wa Facebook aliye kubali kuongelea kuhusu hili hivyo kwa sasa bado hakuna tarehe halisi ya kutoka kwa pesa hiyo au jinsi pesa hiyo itakavyo fanyakazi nje ye mtandao wa Facebook. Kama unataka kujua zaidi kuhusu hili hakikisha unaendelea kutembelea Tanzania Tech tutakujuza yote kuhusu pesa hiyo mpya ya pindi tutakapo pata habari zaidi.